HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 23, 2019

ULEGA UTAFUTWE UFUMBUZI WA NJIA ZA MIFUGO KUINGIA KATIKA MNADA WA IPULI KATIKA MANISPAA YA TABORA

NA TIGANYA VINCENT

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeutaka uongozi wa Mkoa wa Tabora kusimamia ufunguzi njia za muda zinazopendekezwa na wataalamu zitakazotumika kusafirisha mifugo kwenda na kutoka katika Mnada wa Ipuli uliopo kwenye Manispaa ya Tabora ili kuwarahishia wafanyabiashara kutekeleza majukumu yao na kuondoa migogoro baina yao na Manispaa.

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kukutana na wadau wa sekta ya mifugo katika Manispaa ya Tabora, Halmashauri ya Wilaya ya Tabora-Uyui, viongozi wa Chama cha Mapinduzi(CCM) , na viongozi wa Mkoa wa Tabora.

Alisema wakati suluhisho la kudumu likitafutwa juu ya kuendelea au kutendelea kwa Mnada wa Ipuli kuwepo mahali ulipo hivi sasa ni vema mapendekezo yaliyotolewa na wataalamu ya kuwa na njia mpya ya kupeleka mifugo mnadani baada ya ile ya zamani kuvamiwa na kujengwa ni vema Mkoa kwa kushirikiana na wadau kuangalia uwezekano wa kutumia njia hiyo.

Ulega aliongeza kuwa ni pamoja na kuwaondoa watu wote waliopo katika njia ya Mgogoro uliojitokeza kati ya wafanyabiashara wa mifugo

Aidha aliutaka uongozi wa Mkoa wa Tabora kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha wanaweka alama ambazo zitasaidia kuonyesha vivuko vya mifugo ambazo zitasaidia kuepusha mifugo kugonga na magari na wakati mwingine mifugo kukamatwa kwa kuvuka sehemu isiyo rasmi na hivyo kuwasababishia hasara wafugaji.

Naibu Waziri huyo aliutaka uongozi wa Manispaa ya Tabora kuratibu vizuri zoezi la kuwakamata wafugaji wanaovunja Sheria bila kuwaonea na kuwanyanyasa na kuongeza zoezi hilo lazima lizingatie taratibu na sheria zilizopo.

Katika hatua nyingine ameziagiza Halmashauri kuanzisha minada midogo katika maeneo yote ambayo wameyaanisha wakati wakisubiri kupandishwa madaraja kwa kuwa ni kazi rahisi kuanza na mnada mkubwa kama ulivyo wa Ipuli mara moja.

Alisema ili kuanzisha Mnada mpya zinahitajika kiasi cha shilingi milioni 650 ili kukamilisha Mnada sawa na ule wa Ipuli na kuongeza kuwa ujenzi wa uzito tu unagharimu milioni 250 na fedha nyingine ni kwa ajili ya miundo mbinu mingine.

Ulega aliongeza kuwa vigezo kingine ni pamoja na kuwepo na wateja na miundo mbinu inayovutia wafanyabiashara wa mifugo na wadau lazima washirikishwe na wakubaliane.

Awali viongozi wa Halmashauri zote walionyesha sehemu ambazo wako tayari kuanzisha Mnada ambao uyui walimuonyesha eneo la Ilolanguru lenye ukubwa wa ekari 30 na linguine la Kinyamwe –Magiri lenye ukubwa wa ekari 600.

Kwa upande wa Manispaa ya Tabora , uongozi wa Kata ya Misha ulisema uko tayari kutoa eneo la ekari 20 kwa ajili ya uanzishwaji wa Mnada mpya ili kuhamisha ule wa Ipuli kutokana na kukua kwa mji wa Tabora.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri aliwataka wafanyabiashara wa mifugo kuendelea kufanyakazi zao kwa kuzingatia Sheria zinazosimamia Manispaa ya Tabora ya kukataza mifugo kuzurura ovyo katikati miji.

Alisema mifugo ambayo itakutwa ikizurura katikati ya mji na maeneo ya huduma za jamii, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mhusika.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Uyui Lubasha Makoba alisema utatuzi wa tatuzi hilo umesaidia kujenga imani kwa wafanyabiashara wa mifugo na kuepusha kudonda kwa uchumi.

Alimuomba Naibu Waziri kuangalia uwezekano wa kuanzisha Mnada katika maeneo mengine wilayani Uyui.

Naye Mfanyabiashara wa Mifugo Nguji Matemi alisema kumalizika kwa mvutano baina ya wafanyabiashara na uongo umesaidia kurudisha baadhi ya wenzao ambao walikuwa wanakusudia kuachana na biashara katika eneo hilo.

Alisema hatua hiyo imeonyesha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasikiliza kero za watu mbalimbali bila ubaguzi.

No comments:

Post a Comment

Pages