HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 01, 2019

Wambura arejea kortini, apiga hodi FIFA

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kulia ni wakili wake, Emmanuel Muga. (Picha na Francis Dande).

NA JOHN MARWA



MAKAMU wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura, amesema anarejea Mahakamani na kisha kutinga Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kutoa ufafanuzi juu ya sakata lake la kufungiwa.


Awali, Wambura alifungiwa na Kamati ya Maadili ya TFF kujishughulisha na masuala ya soka maisha na kisha Kamati ya Rufaa ya Maadili nayo ikaunga mkono, kabla ya uamuzi huo kutenguliwa na Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, mwishoni mwa mwaka jana.


Baada ya uamuzi huo wa Mahakama, TFF ilipeleka hukumu ya Kamati zake kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), iliyo chini ya Anin Yeboah wa Ghana, kukazia.


Januari 22, Kamati hiyo ya FIFA ikikazia hukumu iliyotolewa Aprili 6, 2018 na Kamati ya Rufani ya Maadili ya TFF.


Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Wambura alisema baada ya kupokea nyaraka kutoka FIFA ya kukazia adhabu ya Kamati ya Maadili ya TFF na Kamati ya Rufaa ya TFF, aliweza kuomba sababu za FIFA kukazia adhabu hiyo.


“Baada ya kupokea nyaraka kutoka FIFA iliyoonyesha FIFA kukazia hukumu ya Kamati za TFF zilizonifungia…Kwa taratibu, sheria na kanuni za FIFA, inatakiwa ndani ya siku 10 uwe umeomba kupata maelezo ya FIFA juu ya maamuzi yao.


“Niliomba na FIFA walinijibu kwa kueleza kuwa wamefanya hivyo kutokana na maelezo yaliyotumwa na TFF, vile vile TFF hawakuwaeleza kuwa nilikuwa nimekata rufaa yoyote, lakini TFF kwa mujibu ya nyaraka hizi, pia hawakuwaleza nilikata rufaa Mahakamani na maamuzi ya Kamati ya Rufaa na Kamati ya Madili ya TFF kutenguliwa,” alisema Wambura na kuongeza.


Sasa kwa kufanya hivyo, FIFA walibaki kwenye maamuzi yaliyotumwa na TFF, kuna mambo mawili yanapaswa kufanyika, moja ni kuwaarifu FIFA uamuzi waliotumia ni uamuzi uliokwisha futwa na Mahakama, hivyo utekelezaji wa adhabu hiyo hautakuwa na madhara ya kisheria nchini Tanzania kwa sababu Tanzania inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria na Katiba yake.


“Jambo la pili ni kurudi tena Mahakamani kuiambia Mahakama, kuna Binadamu mmoja huko amekataa kuheshimu maamuzi ya Mahakama Kuu ya Tanzania, sasa tunaiomba Mahakama kwa mujibu wa Sheria zilizopo, yule mtu aliyekiuka maamuzi ya Mahakama sheria zinasemaje,” alibainisha Wambura.


“Tulichokifanya ni kimoja tu, tumeiomba Mhakama Kuu iwaite ambao wamekaidi maamuzi ya Mahakama kwa makusudi na kuidharau Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili waileze Mahakama kwa nini wasichukuliwe hatua.


“Tayari tumerudisha Mahakamani na Mahakama imepanga kusikiliza Februari 11 mwaka huu, na anayepaswa kwenda kujibu tumeiomba Mahakama, binafsi awe ni Rais wa TFF Wallace Karia,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment

Pages