Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya, akizungumza katika harambee ya uchangiaji wa miundombinu na majengo ya Shule Ulanga.
Viongozi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja.
Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mahenge resources, Hekima Raymond, akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya (kushoto) hundi ya sh. Milioni 16 iliyotolewa na Kampuni hiyo kwaajili ya majengo ya shule wilayani Ulanga.
NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Kinywe (Mahenge Resources)
imechangia sh. Milioni 16 ili kuboresha majengo na miundombinu ya shule
zilizoko katika Wilaya ya Ulanga, Mkoani Morogoro.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi fedha hizo, Mkuu
wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya, aliipongeza na kuishukuru kampuni ya
Mahenge Resources kwa ushirikiano wake endelevu katika shughuli za maendeleo
wilayani humo.
“Naamini kwamba mshikamano uliojengeka kati ya serikali ya
Wilaya yetu na Kampuni hii utachangia sana kuleta manufaa mengi zaidi huko
mbeleni kwa maslahi ya pande zote mbili,”
“Inatia moyo kuona wawekezaji wakubwa wa kiwango hiki
wanaona umuhimu na haja ya kushiriki kwa vitendo maendeleo ya jamii
inayowazunguka na ya taifa kwa ujumla,”alisema DC Ngollo.
Naye Makamu wa Rais wa Mahenge Resources, Hekima Raymond,
alisema wanachofanya ni kuwekeza kwa ajili ya maendeleo ya Watoto na taifa.
“Pia tufanya uwekezaji chanya kwa ajili ya watu
wanaotuzunguka ni jambo ambalo tumelipa kipaumbele cha muda wote kwenye malengo
wakati wote kwa muda mrefu, na hata katika utaratibu wetu wa kurudisha manufaa
kwa jamii, almaarufu kama CSR,”alisema Raymond.
Aidha alisema kwamba kiasi cha fedha walichochangia ni
takribani asilimia 18 ya fedha zote zilizopatikana katika harambee hiyo maalumu
iliyoendeshwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Stephen Kebwe.
“Haya ni majitoleo makubwa toka kwa kampuni yetu,
ikizingatiwa kwamba hata hatujaanza hatua ya ujenzi wa mgodi wenyewe wala
uchimbaji wa kibiashara utakaoiingizia kampuni faida. Wakati tunashugulikia
hatua za leseni na vibali vya uchimbaji, pamoja na kukamilisha uwezo wa kifedha
kwa ajili ya uchimbaji, tutaendelea kutilia mkazo maendeleo ya jamii
inayotunzunguka sambamba na ukamilishwaji wa hatua ya utekelezaji wa sera ya
fidia,uhamishaji na urasimishaji makazi, ili kuendeleza manufaa chanya kwa
jamii,”alisema.
Raymond pia alisema kwamba wataendelea kushirikiana na
serikali katika ukamilishwaji wa leseni na vibali kwani utekelezaji wa mradi ni
suala linalohitaji kukamilishwa kwa usawa kwa maslahi ya pande zote, ili
kuendeleza tija.
Kampuni hiyo imeendelea kutoa chakula cha mchana kwa
wanafunzi wa baadhi ya shule za vijijini ili kupunguza tatizo la utoro
mashuleni ambalo mara kadhaa limeonekana kuwa tishio ikiwemo kudhamini
wanafunzi 100 wa sekondari wanaotoka kaya masikini na kusaidia upatikanaji wa
maji safi na salama kwa shule zenye changamoto.
Mahenge Resources inamiliki kwa asilimia 100 mradi mkubwa wa
madini ya kinywe ulioko Wilayani Ulanga ambapo mradi huo umevuka hatua ya
upembuzi yakinifu, Oktoba mwaka jana, na kusajili maombi rasmi kwa ajili ya
leseni za uchimbaji.
No comments:
Post a Comment