Meneja Mkuu wa Kampuni ya Bima ya CRDB, Arthur Mosha, akizungumzia mashindano ya mbio yaitwayo CRDB Bima Marathon zitakazofanyika Machi 30, 2019 jijini Dar eS Salaam.
NA MWANDISHI WETU
BENKI ya CRDB imeandaa mashindano ya mbio fupi na ndefu yaitwayo Bima Marathon yatakayofanyika jijini Dar es Salaam Machi 30, 2019.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Bima ya CRDB, Arthur Mosha alisema mbio hizo zitaanzia na kuishia kwenye viwanja vya Mlimani City jijini humo.
Alisema washiriki ni watu wote wenye afya njema ambao watajisajili kwenye dawati Maalum lililopo kwenye benki ya CRDB tawi la Mlimani City.
Mosha alisema mwisho wa usajili ni Machi 28 huku akiwasisitiza wakazi wengi wa Dar es Salaam kushiriki kwenye mbio hizo.
"Washiriki watachagua wanataka kushiriki mbio zipi... kuna kilometa nne, kilometa 10 na kilometa 21 na zote hizo wakimbiaji wataanzia palepale Mlimani City na kuishia hapohapo.
"Hizi mbio zitafanyika baada ya mkutano mkubwa wa Bima utakaowashirikisha wadau wa sekta hiyo kutoka nchi mbalimbali Afrika," alisema Mosha.
Alisema lengo la mkutano na mbio hizo ni kiwahamasisha wananchi kutumia huduma mbalimbali za bima zinazotolewa na kampuni yake na kusema zipo faida kubwa kwa wanaotumia huduma za bima.
Kwa mujibu wa meneja huyo zawadi kwa washiriki wote watakaomaliza mbio ni medali huku akisema zawadi nyingine kwa washindi zitatangazwa hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment