HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 24, 2019

BONDIA WA TANZANIA HASSAN MWAKINYO AZIDI KUTAMBA ANGA ZA KIMATAIFA

NA MWANDISHI WETU

HASSAN Mwakinyo oyeeeee! Tanzania oyeeee! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya bondia huyo kumtwanga mpinzani wake, Sergio Gonzalez raia wa Argentina kwa TKO.

Katika pambano hilo la raundi nane lililopigwa jijini Nairobi, lilimshuhudia Mwakinyo akiibuka mbabe raundi ya tano tu baada ya kurusha makonde mfululizo ambayo yalimshinda mpinzani wake huyo.

Mchezo ulianza taratibu katika raundi ya kwanza na ya pili, huku mabondia wote wakionekana kusomana mbinu wakati kila mmoja wao akijilinda zaidi hali iliyofanya mchezo kuwa wa pande zote mbili.

Hadi raundi ya pili inamalizika, Mwakinyo alionekana kushindwa kupenyeza makonde kwenye uso wa Gonzalez ambaye alionekana kujilinda vyema.

Zikiwa zimesalia sekunde chache kumalizika kwa raundi ya tatu, Mwakinyo alicharuka na kumrushia makonde mfululizo mpinzani wake hali iliyoufanya umati wa mashabiki kwenye Ukumbi wa KICC kuripuka kwa hoi hoi, nderemo na vifijo.

Gonzalez alirudi kwa kasi ya ajabu katika raundi ya nne kwa kumshambulia Mwakinyo mfululizo, huku akirusha mkonde kwa mkono wake wa kushoto ulioonekana kuwa na nguvu muda wote wa mchezo.

Wakati kila shabiki akiamini kuwa huenda pambano hilo lingeamuliwa kwa pointi, Mwakinyo alirudi kwa kasi ya ajabu katika raundi ya tano na kurusha makonde mfululizo ambayo yalimshinda Gonzalez.

Mwakinyo alionekana kutumia vyema udhaifu wa Gonzalez upande wake wa kushoto ambao alikuwa akiulinda muda mwingi wa mchezo.

Makonde mawili ya nguvu kutoka kwa Mwakinyo yalitosha kumpeleka chini Gonzalez ambaye alishindwa kunyanyuka hali iliyomfanya mwamuzi kuamuru kumalizika kwa pambano hili.


Kufuatia ushindi huo, maelfu ya mashabiki waliofurika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kombezi jijini Tanga, uliripuka kwa hoi hoi, nderemo na vifijo.

Umati huo wa wana Tanga ulikusanyika katika maeneo ya Makorora ambapo ndipo Mwakinyo alipozaliwa ili kumuunga mkono kijana wao huyo ambaye ni balozi wa kampuni ya SportPesa.

Kila mmoja aliyefika uwanjani hapo alionekana kurekodi kilichokuwa kikijiri kwenye runinga kubwa iliyotumika kurusha mchezo hiyo kwa kutumia simu yake ya mkononi huku furaha ikitanda kila kona.

Hili litakuwa ni pambano la 15 kwa Hassan Mwakinyo kuibuka na ushindi baada ya kushuka ulingoni mara 17 katika mapambano ya kulipwa, huku akipoteza mawili tu kati ya hayo tangu alipoanza kujihusisha rasmi na ngumi za kulipwa mwaka 2015.

Mtanzania mwingine, Iddi Mkwera, alimchapa Mkenya Nicholas Mwangi kwa TKO katika pambano la utangulizi la kumsindikiza Fatuma Zarika na Catherine Phiri wa Malawi la kuwania ubingwa wa dunia wa WBC kwa wanawake.
 
 Sergio Gonzalez akikwepa ngumi ya Hassan Mwakinyo.
 Hassan Mwakinyo akitupiana makonde na mpinzani wake.
 Sergio Gonzalez akijihami.
 Mwakinyo akirusha makonde mazito kwa mpinzani wake.

 Mwamuzi akimwokoa bondia wa Argentina Sergio Gonzalez.
 
 Bondia wa Argentina Sergio Gonzalez akiwa chini baada ya kupata kichapo kikali kutoka kwa bondia wa Tanzania Hassan Mwakinyo.
 Bondia wa Argentina Sergio Gonzalez akiwa chini baada ya kupata kichapo kikali kutoka kwa bondia wa Tanzania Hassan Mwakinyo.
 Mwamuzi akihesabu kabla ya kumaliza pambano.
 Sergio Gonzalezakiwa hoi.
 Mwamuzi akimaliza pambano hilo baada ya
Sergio Gonzalez kushindwa kuendelea katika raudi ya 5.
 Hassan Mwakinyo akiwa na wasaidizi wake.
 Mwamuzi akimtangaza mshin di wa pambano hilo bondia Hassan Mwakinyo kutoka Tanzania.
Sergio Gonzalez akisaidia kutoka katika ulingo baada ya kuchapwa katika raaundi ya 5
Mwakinyo akipongezwa.

No comments:

Post a Comment

Pages