HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 26, 2019

HUDUMA BORA ZA NMB ZAMKUNA WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Albert Jonkergouw, katika futari iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa Masheikh wa Mikoa ya Kanda ya Kati, Wazee wa Dodoma, Wabunge, Viongozi wa Dini, Wananchi, wawakilishi wa Taasisi mbalimbali na wafanyakazi wa NMB kwenye hoteli ya Dodoma juzi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika futari iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa Masheikh wa Mikoa ya Kanda ya Kati, Wazee wa Dodoma, Wabunge, Viongozi wa Dini, Wananchi, wawakilishi wa Taasisi mbalimbali na wafanyakazi wa NMB kwenye hoteli ya Dodoma juzi.

NA SALUM MKANDEMBA

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameitaja benki ya NMB kuwa ni taasisi inayopaswa kuigwa kutokana na ubora wa huduma, huku akisifia namna walivyoweka mizizi katika maeneo ya vijijini ambako taasisi nyingi za kifedha hazijafika.

Majaliwa alitoa kauli hiyo juzi katika Hoteli ya New Dodoma, wakati benki ya NMB ilipowakutanisha wadau kutoka mkoani humo kwenye futari maalum kwa ajili ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Waziri Mkuu alisema NMB inaisaidia Serikali katika juhudi za maendeleo hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linaelekea katika Uchumi wa Kati, hivyo akaomba Watanzania kwa umoja wao kudumisha, amani, upendo na mshikamano ili kufikia malengo.

Alisema Serikali ambayo ina hisa ndani ya benki hiyo, itaendelea kushirikiana nao pale wanapoona inafaa kufanya hivyo, lakini akawataka waendelee kuboresha zaidi huduma zao katika maeneo ambayo hawajafika.

“Siyo dhambi nikisema mnaongoza kwa kutoa huduma bora, nawashukuru kwa kujikita katika taasisi kama mashule ambako mmesaidia kupeleka madawati na vitabu, lakini nafurahi kusikia mmeanza kufadhili hadi kwenye michezo, nawapeni hongera, tutaendelea kuwatia moyo popote mlipo,” alisema Majaliwa.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, aliwataka NMB kutangaza huduma yao ya mikopo kwa wakulima ambayo yeye (Pinda) alishaelezwa na kuona ina faida kubwa ili jamii ya wakulima waielewe na kuitumia fursa.

Pinda alisema amekuwa miongoni mwa wakopaji wa mara nyingi katika benki hiyo, ndipo maofisa kutoka benki hiyo wakamtembelea na kumpa ushauri kuhusu mkopo maalumu kwa wakulima ambao hauwezi kumuumiza akitumia dirisha hilo.

Kwa mujibu wa Mstaafu huyo, hakuna foleni wala njoo kesho wakati mtu anahitaji mkopo ndani ya benki hiyo, ilimradi mhusika akitimiza masharti ya dhamana zake.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Albert Jonkergouw, alisema benki hiyo inajishusha kwa kuwakumbuka waumini katika kipindi hiki ambacho wanatimiza moja ya nguzo za dini yao ya Kiislamu, hivyo wanaungana katika tendo hilo jema.

Joukergouw alisema wataendelea kufanya hivyo na kufuata taratibu za huduma za fedha nyingi, ikiwemo kuwasogezea zaidi huduma watu ambao wamekuwa wakizitafuta kwa gharama.

Mkurugenzi huyo akahitimisha kwa kuahidi benki yake kuendelea kufuturisha waumini wa Kiislamu, wateja wao na waalikwa wengine, na watahitimisha hafla za kufuturisha hapo Mei 31 mkoani Tabora, lakini kila mkoa wanatumia nafasi hiyo kuwaalika na wawakilishi kutoka maeneo ya jirani.

No comments:

Post a Comment

Pages