.Zitatolewa Siku ya Maadhimisho ya Bima Sept. 27
.Wasomi na wataalamu 8 waunda jopo la majaji
NA DEODATUS MKUCHU
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli
za Bima (TIRA), Dk. Baghayo Saqware amesema mamlaka hiyo haitasita kuzifungia
kampuni za bima zinazokiuka sheria kwa kufanya udanganyifu na kutoa huduma chini
ya kiwango.
Dk. Saqware ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzindua wa tuzo za umahiri katika sekta ya Bima katika kutambua
kampuni za bima na bidhaa zake pamoja na juhudi za watu binafsi waliosaidia
kutoa mchango wa ukuzaji wa sekta hiyo nchini.
Alisema sekta ya bima nchini inawajibu mkubwa
katika kukuza, kuendeleza na kuondoa umaskini wa kiuchumi kwa taasisi na watu
binafsi hivyo ni muhimu zikafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria.
"Sekta imara ya bima husaidia na kuvutia
wawekezaji kufanya biashara bila hofu hivyo kuendeleza uchumi, sekta hii pia
ina mchango mkubwa katika kuendeleza viwanda na kutekeleza kwa vitendo kauli
mbinu ya serikali ya awamu ya tano ya kuendeleza viwanda na uchumi nchini,
" alisema.
Kuhusu tuzo, Dk. Saqware alisema tuzo hizo zitazotolewa kwa mara ya kwanza tangu
kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo, pia zimelenga kuzitambulisha shughuli za bima kwa
wananchi ambao wengi wao bado haijawa na uelewa wa kutosha kuhusiana na masuala
ya bima.
Alisema tuzo hizo zenye lengo la kuendeleza weledi
wa taaluma ya bima na soko la bima kwa kubainisha, kuthamini, kutambua mchango
wa kampuni hizo pamoja na bidhaa zilizofanya vizuri katika soko, zitasaidia
uhimarishaji na ukuaji wa sekta hiyo katika kuendeleza shughuli za kiuchumi na
kijamii kwa wananchi.
Aidha, alisema tuzo zinazowaniwa katika mchakato
huo kuwa ni pamoja na tuzo ya umahiri katika elimu, itakayotolewa kwa kampuni
inayotoa elimu kwa umma yenye tija na tuzo ya umahiri katika utoaji wa huduma
itakayotolewa kwa kampuni inayotoa misaada kwa wananchi katika sekta ya afya.
Nyingine ni pamoja na tuzo ya umahiri kwa kijana
anayeibukia (18-30) itakayotolewa kwa vijana waliotoa mchango katika sekta ya
bima kwa jamii katika nyanja ya aujasiriamali, na utafiti unaohusisha urahisi
wa upatikanaji wa huduma za bima.
Dk. Saqware aliitaja tuzo nyingine kuwa ni tuzo kwa
kampuni bora ya mwaka, itakayotolewa kwa kampuni bora miongoni mwa kampuni za
bina nchini.
Tuzo nyingine ni ya umahiri katika bidhaa bora na
yenye ubunifu inayotolewa kwa kampuni inayotoa bidhaa iliyobuniwa vizuri na
kumnufahisha mwananchi hususani wa vijijini na yenye gharama nafuu.
Aidha, alisema mchakato wa tuzo hizo utakaohusisha
majaji nane unatarajiwa kuanza Juni 28 Mwaka huu kwa washiriki kutuma maombi
kabla ya kufanyika kwa mchakato wa wananchi kuwapigia kura washiriki
unaotarajiwa kufanyika katika ya Septemba Mosi hadi 21 Mwaka huu.
Majaji waliokabidhiwa
jukumu hilo zito, ni Peter Ilomo (Mwenyekiti), Rajab Kakosa (Makamu), Dk. Jamal
Katundu (Katibu), Oktavian Mshiu, John Ulanga, Neema Kiure Msusa, Sanjay
Rughani na Louis Accaro.
Alisema washindi watakaopatikana chini ya jopo hilo
lililosheheni wataalamu na wazoefu wa fani mbalimbali, watatangazwa na kupewa tuzo
zao siku ya maadhimisho ya Siku ya Bima nchini yatakayofanyika Septemba 27,
jijini Mwanza.
Alizitaja zawadi zitakazotolewa kwa washiriki bora
katika vigezo 11, ni pamoja na vikombe na vyeti kwa lengo la kupanua wigo wa
upatikanaji wa huduma za bima nchini kuelekea uchumi wa Kati.
Aidha, ni kuhakikisha sekta ya bima inaendeshwa kwa
weredi wa hali ya juu kuondoa matapeli waliovamia na kuchafua taswira ya huduma
hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi na watu wake.
Kwa upande wa maadhimisho ya Siku ya Bima, ni mara
ya tatu kufanyika nchini ambapo katika miaka miwili iliyopita 2017 na 2018,
yalifanyika jijijini Tanga.
Katibu wa Taasisi ya Bima Tanzania, Ernest Kilumbi, akizungumza kabla ya kumkaribisha rais wa taasisi hiyo, Bosco Bugali, kutoa hotuba yake wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Tuzo za Umahiri wa Kampuni za Bima uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. (Picha na John Dande).
Rais wa Taasisi ya Bima Tanzania, Bosco Bugali (katikati), akizungumza wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Tuzo za Umahiri wa Kampuni za Bima uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu wa Taasisi ya Bima Tanzania, Ernest Kilumbi na kulia ni Kamishna wa Bima nchini, Dk. Barghayo Saqware.
Kamishna wa Bima nchini, Dk. Barghayo Saqware, akizungumza wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Tuzo za Umahiri wa Kampuni za Bima uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya majaji watakaosimamia mchakato wa tuzo hizo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakichukua taswira.
Picha ya pamoja.
No comments:
Post a Comment