Na Makuburi Ally, Mtwara
OMBI la mirathi kati ya Mohamed Mussa dhidi ya Jamaldin Mtonya na Kuruthum Mtonya linatarajia kusikilizwa Juni 11, 2019 Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara.
Shauri hilo lililokuwa lianze kusikiliza ombi la mirathi Mei 9 halikuskilizwa kwa Sababu ya kukosekana kwa mpingaji wa ombi la usimamizi wa mirathi hiyo, Jamaldin Mtonya aliyeumwa Malaria na kutuma mwakilishi ambaye ni Hassan Salum Namkami aliyewakilisha taarifa za kuumwa kwake.
Katika shauri hilo linalosimamiwa na Jaji Wilfred Dyansobera baada ya kupokea taarifa hiyo, alimuuliza mwakilishi kwamba umekuja na cheti kinachoelezea kuumwa kwa Jamaldin, akaeleza mahakamani hapo kwamba hakuja nacho.
Baada ya kujibiwa hivyo, Jaji Dyansobera alimuuliza Mohamed Mussa wachukue hatua gani baada ya kukosekana kwa mpingaji, akajibu anaiachia mahakama iamue.
Swali kama hilo akaulizwa pia Kuruthum naye akajibu kwamba mahakama ndio yenye uamuzi kuhusu mwenendo wa kesi hiyo ndipo jaji akaeleza kwamba shauri hilo litasilikizwa Juni 11 mwaka huu.
Kabla ya Mei 9 mlalamikaji Mohamed Mussa aliwasilisha rufaa mahakamani hapo baada ya Mahakama ya Wilaya Tandahimba kutomtendea haki aliyoitaka ikiwemo kutoa hukumu iliyotolewa Oktoba 27, 2018 ambayo ilikuwa siku ya Jumamosi siku ambayo si ya kazi.
Baada ya Mohamed Mussa kuwasilisha maombi ya kuwa msimamizi wa mirathi hiyo, Jaji Dyansobera aliwataka walalamikiwa kuwasilisha mapendekezo yao kuhusu usimamizi wa mirathi hiyo jambo ambalo walilitekeleza.
Rufaa hiyo yenye namba 23/2018 inahusu usimamizi wa mirathi ya marehemu Mussa Mtonya ambaye alikuwa na mashamba makubwa likiwemo la ukubwa wa ekari 118, ekari 80 na mali nyinginezo.
Awali mvutano wa pande hizo mbili umetokana na mlalamikaji, Mohamed Mussa kuomba kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu baba yao aliyefariki dunia mwaka 2002 ambaye aliacha watoto 20.
Katika hoja zake mahakamani hapo, Jamaldin anapinga kaka yake Mohamed kuwa msimamizi wa mirathi hiyo na kuhitaji dada yake Kuruthumu Mussa ndiye awe msimamizi wakati hajawasilisha maombi ya kutaka kufanikisha hatua hiyo.
Katika Rufaa yake hiyo Mahakama Kuu, Mohamed Mussa anaeleza kwamba kwa kuwa yeye ameomba kusimamia mirathi ya marehemu baba yake, ndio maana aliwasilisha maombi hayo tangu mahakama ya mwanzo iliyoko wilayani Tandahimba mkoani Mtwara lakini dada yake hakuomba lakini anashangaa wanamlazimisha.
Kwa upande wake Kuruthum amewasilisha ombi la kukataa kuwa msimamizi wa mirathi hiyo kwa sababu hakuhitaji kutekeleza hatua hiyo ambayo inawezekana ikatekelezwa na kaka yake.
No comments:
Post a Comment