HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 14, 2019

MAKATIBU WA MAWAZIRI NA MAKATIBU WA NAIBU MAWAZIRI WAPATIWA MAFUNZO ILI KUWAJENGEA UWEZO KIUTENDAJI

 Mratibu wa Wasaidizi wa Viongozi, Bw. John Kiswaga akiwasilisha hoja kwa Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji yaliyofanyika jijini Dodoma leo.


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Makatibu wa Mawaziri na wa Naibu Mawaziri wamepatiwa mafunzo ya siku moja na Serikali ili kuwajengea uwezo kiutendaji.

Akifungua mafunzo hayo leo jijini Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael amesema, watumishi hao wanapaswa kuzielewa vema Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma pamoja na mipaka ya kazi zao ili waweze kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wao.

“Mafunzo hayo yatawaongeza upeo na uelewa wa majukumu yao katika utendaji kazi.” Dkt. Michael amesisitiza.

Dkt. Michael ameongeza kuwa, serikali inaandaa utaratibu wa kuwa na mafunzo endelevu ya namna hiyo kwa Makatibu hao.

Aidha, Dkt. Michael amefafanua kuwa, serikali imeona kuna umuhimu wa kuandaa waraka na mwongozo utakaoonyesha stahili na majukumu ya Makatibu hao katika mizania moja kutokana na utofauti wa kiutendaji katika Wizara.

Naye, Mratibu wa Wasaidizi wa Viongozi, Bw. John Kiswaga amesema, mafunzo hayo yatasaidia kuwakumbusha umuhimu wa utekelezaji wa miongozo ya serikali ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya viongozi.

Mafunzo ya Makatibu wa Mawaziri na Makatibu wa Naibu Mawaziri yameandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo mada mbalimbali zimewasilishwa.

No comments:

Post a Comment

Pages