Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Jaji Mstaafu Januari Msoffe
akimkabidhi Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Augostine Mahiga moja ya Ripoti
tatu zilizofanyiwa utafiti na Tume hiyo kuhusiana na eneo la Hifadhi ya Ngorongoro,
Sheria ya Ushahidi na Sheria ya Ufilisi jijini Dodoma tarehe 13 Juni 2019. Kushoto
ni Katbu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sufini Msoffe. (Picha na Munir Shemweta).
Na
Munir Shemweta, Dodoma
Tume ya Kurekebisha
Sheria Tanzania imekabidhi Ripoti ya Mapitio ya Sheria ya eneo la hifadhi ya
Ngorongoro lilipo mkoani Arusha kwa Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Agostine
Mahiga.
Aidha, Tume imekabidhi
pia Ripoti mbili za Sheria ya Ufilisi na ile ya Ushahidi ambazo zote kwa pamoja
zimekabidhiwa kwa Dkt Mahiga na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji
Mstaafu Januari Msoffe leo tarehe 13 Juni 2019 jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa
kukabidhi Ripoti hizo, Mwenyekiti wa Tume Jaji Mstaafu Januari Msoffe alisema
Tume yake imeamua kufanya utafiti wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro baada ya
kuombwa na Mamlaka ya Ngorongoro kufanya utafiti kutokana na eneo hilo kuruhusu
matumizi mseto ambapo Wanyama pori, Mifugo na Binadamu wanaishi eneo moja.
Jaji Mstaafu Msofe
alisema, eneo la Hifadhi ya Ngogongoro ni hifadhi ya pekee inayoruhusu matumizi
mseto yanayojumuisha watu, mifugo na wanyama pori na kusisitiza kuwa Tume yake
wakati wa kupitia sheria hiyo imebaini upungufu wa kisheria na kiutendaji.
Alisema, katika utafiti
huo Tume ya Kurekebisha Sheria ilibaini ongezeko kubwa la idadi ya watu katika
mhifadhi hiyo ambapo mwaka 1959 hifadhi hiyo ya Ngorongoro likuwa na idadi ya
watu 8,000 wakati sasa ina takriban wakazi 93,000 jambo alilolieleza kuwa linahatarisha
kupungua kwa malisho ya wanyama, uharibifu wa mazingira pamoja na kuharibiwa
kwa mapito ya wanyama.
Aidha, Mwenyekiti huyo
wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania alisema, hifadhi hiyo ya Ngorongoro pia
imeathiriwa na usajili wa vijiji ndani ya hifadhi pamoja na ujangili jambo alilosema
limesababisha kupungua wanyama pori wakiwemo Faru na Mbwa mwitu.
Jaji Mstaafu Msoffe
aliongeza kwa kusema, Tume yake inapendekeza hatua za kuangalia mfumo wa
matumizi Mseto katika hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuhakikisha eneo hilo
linakuwa endelevu.
Kwa upande wake Waziri
wa Katiba na Sheria Balozi Agostine Mahiga aliipongeza Tume ya Kurekebisha
Sheria kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kufanya tafiti katika sheria mbalimbali
na kueleza kuwa chombo hicho ni muhimu katika nchi kwa kuwa kinabeba majukumu
ya masuala ya sheria ili yasije kupitwa na wakati na kubainisha kuwa Tume ina macho
matatu katika utendaji wake ambapo inaangalia sheria zilizopo, zilizopita na
zijazo.
No comments:
Post a Comment