Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania
(TFCG), Emmanuel Lyimo, akizungumza na maofisa misitu, maliasili, kilimo,
ardhi, sheria na maendeleo ya jamii kutoka wilaya 16 baada ya kufanya
ziara ya siku tatu kujifunza kuhusu Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta
ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu 'Mkaa Endelevu' unaotelekezwa katika
wilaya Kilosa, Mvomero, Morogoro mkoani Morogoro. (Picha na Suleiman
Msuya).
Na Suleiman Msuya
MAOFISA
misitu, maliasili, ardhi, kilimo, maendeleo ya jamii kutoka wilaya 16
nchini wameiomba Serikali kuandaa muongozo ambao utaelekeza halmashauri
kutenga bajeti kwa ajili ya usimamizi misitu ya vijiji kuwa endelevu.
Maofisa
hao wametoa ombi hilo baada ya kumaliza ziara ya siku tatu
iliyoandaliwa na Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania
(TTCS) maarufu 'Mkaa Endelevu'iliyofanyika katika vijiji vya Matuli na
Mlilingwa wilayani Morogoro mkoani Morogoro.
Mradi
wa TTCS unatekelezwa katika vijiji 30 vya wilaya za Kilosa, Mvomero na
Morogoro chini ya usimamizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili
Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania
(Mjumita), Shirika la Kuendeleza Nishati Asili (TaTEDO) chini ya
ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).
Akizungumza
baada ya kumaliza ziara hiyo Ofisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya ya
Liwale, Damas Mumwi alisema iwapo kutakuwa na maagizo kutoka juu kuhusu
uwekezaji wa misitu ni dhahiri uendelevu utakuwepo.
Mumwi alisema iwapo misitu ya vijiji na maliasili zitaangaliwa na halmashauri pekee kuwa uwezekano wa kumalizika.
"Tumeona
maendeleo yaliyopatikana kupitia Usimamizi wa Shirikishi wa Misitu
(USM) kwenye vijiji hivi nashauri kama Serikali kupitia wizara husika
inatoa muongozo kwa halmashauri kutenga bajeti ya USM kama ilivyofanya
kwa vijana, wakina mama na walemavu," alisema.
Ofisa
Ardhi na Maliasili huyo alisema misitu ni rasilimali muhimu katika
kuchochea maendeleo ila kinachokosekana ni uwekezaji kama TTCS
ilivyofanya Morogoro.
Kaimu
Ofisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya ya Mvomero, Sadoyeka Kyaruzi alisema
uwekezaji katika sekta hiyo utasaidia Serikali kuweza kutatua
changamoto za wanavijiji.
Kyaruzi
alisema katika wilaya yao kuna vijiji vitano vilivyopo kwenye mradi
ambapo kumekuwa na mabadililo makubwa ya kiuchumi, kijamii na maendeleo.
"Naomba
kusisitiza bila kuwepo kwa maelekezo kutoka juu kuhusu utengaji wa
bajeti kwa ajili ya USM ni vigumu kupata matoe chanya kwenye sekta hii,"
alisema.
Kwa upande wake
Ofisa Misitu Wilaya ya Tunduru, Paul Onesmo alisema atahakikisha elimu
aliyoipata anaipeleka Tunduru ili mradi huo wa mkaa endelevu utekelezwe.
Onesmo alisema iwapo wafanya maamuzi watakuwa na uelewa kuhusu USM ni dhahiri kuwa misitu itakuwa salama na kuchangia maendeleo.
Solomon
Benjamin Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Ruangwa alisema wilayani
kwao wameshaanza kunufaika na rasilimali misitu hivyo anaamini wakati
muafaka wa kusambaza elimu ya mkaa endelevu kwa kushawishi utengaji wa
bajeti katika usimamizi wa misitu.
Ofisa
Misitu Msaidizi Wilaya ya Songea, Hadija Bakari alisema ziara hiyo
imeonesha matokeo chanya kwake hivyo atatumia kila njia kushawishi
halmashauri kutenga bajeti katika USM.
Bakari alisema pamoja na ushawishi huo anatarajia kutoa elimu kwa wananchi umuhimu wa utunzaji wa misitu kwa dhana ya endelevu.
Gravas
Mwalyonbo Ofisa Misitu Namtumbo alisema mradi huo unapaswa kusambazwa
katika wilaya zote zenye misitu ya vijiji kwani unapunguza uvunaji
haramu wa rasilimali misitu na maliasili.
Alisema
halmashauri zinapaswa kuweka kipaumbele katika sekta ya misitu na
maliasili kama ilivyo kwa elimu, afya, miundombinu na kilimo.
Ofisa
Maendeleo ya Jamii wilaya ya Morogoro alisema Florence Mwambene alisema
mradi huo umesaidia kuondoa changamoto nyingi katika vijiji vilivyo
kwenye mradi.
Mwambene
alisema katika vijiji vya Mlilingwa, Matuli, Diguzi na Tununguo wa
navijiji wameboresha maisha yao kupitia mradi huku uhifadhi ukiimarika.
Meneja
Misitu Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Benadetta Kadala alisema
kiujumla mradi umeonesha matokeo chanya ila kinachohitajika ni kuwepo
kwa mipango endelevu baada ya mradi kuisha.
Ofisa
Misitu Mkuu Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii,
Seleboni John alisema yeye kama mtaalam wa misitu ameona manufaa na
kuahidi kufikisha kwa wakubwa zake kuangalia nanma ya kusambaza mradi
huo.
John aliwataka
maofisa hao kuandaa taarifa sahihi kuhusu walichojifunza ili wakurugenzi
na wafanya maamuzi katika ngazi zao waweze kusukuma mbele zaidi.
Mkurugenzi
Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo alisema msingi mkubwa waliotumia
kutekeleza mradi huo ni ushirikiano hivyo kuwaomba maofisa hao waliokuja
kujifunza kutumia njia hiyo kabla ya kuingia katika utekelezaji.
No comments:
Post a Comment