HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 31, 2019

DKT. MPANGO: FANYENI KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI, KANUNI NA TARATIBU ZA UTUMISHI WA UMMA

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akizungumza na Waajiriwa wapya, alipofanya nao mkutano jijini Dodoma na kuwataka waajiriwa hao kufuata maadili ya Utumishi wa Umma. (Picha na WFM).

Na Saidina Msangi na Josephine Majura WFM - Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango awataka Waajira wapya  wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma.

Hayo ameyasema alipofanya nao kikao cha kuwakaribisha wizarani hapo Jijini Dodoma, ambacho kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utawala Dkt. Khatibu Kazungu, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Sera Bw. Adolf Ndunguru na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho Dkt. Mpango alisema kuwa  anatarajia kuona watumishi hao wanafanya kazi kwa kwa bidi na  kujituma,  na kuwa wazalendo kwa nchi yao. 

“Umasikini wa watanzania uwasukume kufanya kazi kwa bidii, nchi ina rasilimali nyingi lakini asilimia 26.4 ya wananchi bado hawapati mahitaji ya msingi hivyo tufanye kazi kwa bidii kusaidia watu kuondokana na umasikini.”Alisisitiza Waziri Mpango.

Aliwataka  Watumishi hao kutumia ujuzi wao kufanya kazi kwa weledi mkubwa kwa hadhi ya kimataifa kwa kuzingatia  uadilifu na uaminifu katika kutekeleza majukumu yao. 

AIDHA, Dkt. Mpango amewataka Viongozi wa Wizara hiyo, kuwapa ushirikiano Watumishi hao na kuwa tayari kuwasaidia na kuwaelekeza katika majukumu yao watakayo wapangia lakini pia wawe tayari kujifunza kutoka kwao.

‘’Muwe tayari kuwasikiliza na kuwasaidia watakapopata changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao”,alisema Dkt. Mpango.

Aliwataka Watumishi hao kuhakikisha wanajiendeleza kielemu wanapopata nafasi na kutoridhika kwa elimu waliyokuwa nayo kutokana na ukuaji wa teknolojia.

Dkt. Mpango alisema Wizara hiyo inamajukumu mengi takribani 20 ikiwemo kubuni na kusimamia sera za bajeti, fedha,ununuzi wa umma pamoja na ubia kati ya sekta za umma na sekta binafsi.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa dira ya Taifa, kupanga na kutekeleza mandeleo ya uchumi yaende wapi, pia  ina jukumu la kuandaa muongozo wa bajeti ya Serikali na utekelezaji wake.

Naye mmoja wa Waajiriwa wapya ameishukuru Serikali kwa kutoa ajira na kuahidi kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia madili ya Utumishi wa Umma.

Jumla ya Watumishi  wapya 70  wa kada mbalimbali  wakiwemo Wachumi na Wasimamizi wa Fedha wameajiriwa katika Wizara  ya Fedha na Mipango ikiwa ni ajira yao mpya.

No comments:

Post a Comment

Pages