Askofu Mku wa Kanisa la Ligthouse Christian Center (LHCC), Dkt. Rejoice Ndalima akiongoza maombi ya kuliombea amani Taifa yaliyofanyika katika kanisa hilo Jumapili, Ubungo jijini Dares Salaam kwa kushirikiana na Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO). Kushoto ni Rais wa TAMUFO, Dkt. Donald Kisanga.
maombi yakiendelea.
Maombi yakiendelea.
Maombi yakiendelea. Kutoka kushoto ni waimbaji wa nyimbo za injili, Upendo Nkone na Bahati Bukuku.
Maombi yakiendelea. Kutoka kushoto ni Waimbaji wa nyimbo za injili, Upendo Nkone, Bahati Bukuku na Stellah Joel ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TAMUFO.
Na Kulwa Mwaibale
UMOJA wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) kwa kushirikiana na Kanisa la Ligthouse Christian Center (LHCC) la Ubungo, Dar wamefanya maombi maalumu ya kuliombea amani Taifa linapoelekea kwenye chaguzi mbalimbali.
Maombi hayo yamefanyika Jumapili katika kanisa hilo na kuhudhuriwa na wasanii maarufu wa Muziki wa Injili wa nchini, nje ya nchi na waumini wa madhehebu tofauti.
Akizungumza kabla ya kuanza maombezi, askofu wa kanisa hilo, Dkt. Rejoice Ndalima ambaye pia ni mlezi wa TAMUFO alisema wameamua kufanya maombi hayo ili nchi yetu iendelee kuwa na amani wakati wote.
“Taifa letu linajiandaa kuingia kwenye chaguzi mbalimbali hivyo hatunabudi kuliombea ili amani itawale,” alisema askofu huyo.
Ndalima aliongeza kuwa nchi isipokuwa na amani hakuna kinachoweza kufanyika, akatoa rai kwa watanzania kuilinda kwa gharama yoyote.
“Leo tutaliombea taifa letu, rais wetu Magufuli tuliyepewa na Mungu, viongozi wetu ambapo tutamsihi Mungu atuepushe na machafuko ya aina yoyote,” alisema Ndalima.
Aidha, alikemea tabia ya baadhi ya watu kuwazushia vifo watu wengine kama ilivyotokea hivi karibuni kwa Msanii Bahati Bukuku aliyezushiwa kafariki dunia.
Akizungumza kwenye tamasha hilo la maombezi lililokwenda sambamba na harambee ya kukusanya pesa kwa ajili ya TAMUFO kwenda kueneza injili Makambako mkoani Njombe, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya utengenezaji vipodozi vya asili ya Grace, Elizabeth Kalili aliyekuwa mgeni rasmi aliwasihi wanamuziki wa injili kupendana.
Kalili alikemea tabia ya wanamuziki hao kuoneana wivu, kusengenyana na kutoshikamana ambapo alisema inasababisha kuurudisha nyuma muziki huo.
“Uiambaji wa muziki wa injili ni kuhubiri neno la Mungu kwa watu, hivyo waimbaji wanatakiwa kupendana siyo kuleteana majungu na unafiki,” alisema Kalili.
Aliongeza kuwa anamuunga mkono Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuiletea nchi maendeleo akawasihi na wengine kufanya hivyo.
Naye Rais wa TAMOFA, Dkt. Donald Kisanga alisema wameamua kuliombea amani taifa kwa sababu nchi yoyote isipokuwa na amani haiwezi kuwa na maendeleo.
“Pasipokuwa na amani hakuna kitu kinachoweza kufanyika, hata sisi TAMUFO na Ligthouse Christian Center tusingeweza kufanya hili tamasha la maombezi ya taifa letu kama pasingekuwa na amani,” alisema Kisanga.
Kisanga ametoa rai kwa watanzania, taasisi za dini, wafanyabiashara, mawaziri, wabunge na watu wa kawaida kuwachangia fedha ili waweze kufanikisha mkutano mkuu wa injili utakaofanyika Makambako mkoani Njombe Septemba mwaka huu.
“Kwa kuwa kupitia TAMUFO Kuna fursa nyingi za watu kupata matibabu kutoka kwa madaktari bingwa wa Hospitali ya Apollo ya nchini India, Marie Stopes na kadhalika, tunaomba sapoti kwa watu mbalimbali ili tuweze kufanikisha mkutano huo,” alisema Kisanga.
Wasanii waliohudhuria tamasha hilo ni Bahati Bukuku, Emmanuel Mbasha, Upendo Nkone, Stella Joel ambaye ni Katibu wa TAMUFO, Msanii Imani Buliga kutoka Jamhuri ya Kidemoksia ya Congo (DRC), Makasi Junior, Kwaya ya Victoria, Sayuni, Ligthouse na wasanii wengine.
No comments:
Post a Comment