Afisa
Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati, Filbert Mponzi kutoka NMB akizungumza
na wachimbaji wadogo wa madini wa mkoa wa Geita, kwenye jukwaa la mtaji
wa Maendeleo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini wa Mkoa wa Geita, kwenye jukwaa la mtaji wa Maendeleo mkoani humo lililodhaminiwa na Benki ya NMB. (Na Mpiga Picha Wetu).
Na Mwandishi Wetu, GEITA
BENKI ya NMB imeahidi kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo zaidi ya
400 mkoani Geita.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja
Wakubwa wa NMB, Filbert Mponzi, alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika Kongamano
la siku tatu la Jukwaa la Mtaji na Maendeleo Geita lililoshirikisha wachimbaji
wadogo zaidi ya 400.
Alisema hadi sasa benki imekopesha
zaidi ya Sh. Bilioni 40 kwa Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati (SME’s) na kuwa
wachimbaji nao ni sehemu ya wanufaika hao.
Aliwataka wachimbaji hao
kujenga tabia ya kufanya biashara zinazozingatia weledi wa kutunza kumbukumbu
za fedha na kufungua akaunti za vikundi, ili kuweka hai nafasi ya kukopesheka
katika taasisi za kifedha nchini kwa ustawi wa biashara zao na taifa kwa
ujumla.
“Kwa sasa changamoto
zinazokwaza wachimbaji ni ukosefu wa akaunti za benki za vikundi, ambazo
zinaweza kuruhusu kukopesheka. Njia sahihi kwenu kwa sasa ni kuunda vikundi na
kujirasimisha, ili kuweza kupata mikopo katika taasisi za kifedha.
“Tunaamini kuwa, iwapo
mtaufanyia kazi ushauri wetu na elimu mliyopata hapa, mkaweka mfumo rasmi wa
kukopesheka kwa mtu mmoja mmoja ama vikundi, tutawaptia mikopo. Tutaendelea
kuelimisha wafanyabiashara ya madini, ili kuwaongezea chachu ya kuweka akiba na
kukuza mitaji,” alisema Mponzi.
Akizungumza wakati wa kufunga
kongamano hilo, Naibu Waziri Madini,
Stanislaus Nyongo, aliipongeza NMB, kuwa benki kinara katika kusaidia harakati
za kijamii na kuwakaribisha Geita kuwaunga mkono wachimbaji wadogo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Injinia Gabriel Luhumbi, aliwataka washiriki waungane na kuunda vikundi imara
vyenye uongozi makini unaotimiza wajibu kulingana na katiba za vikundi.
“Muunganike, muwe na vikundi imara. Mara
nyingi mikopo ya uwezeshaji inakuja kwa vikundi,” alisema.
No comments:
Post a Comment