Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakiwa katika picha ya pamoja na walimu wao baada ya kutunukiwa vyeti vya Shirikisho la Riadha Kimataifa (IAAF) Level 1. (Na Mpiga Picha Wetu).
Na Makuburi Ally
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimewataka viongozi wa
Vyama na Mashirikisho ya michezo nchini kushirikiana nacho kwa lengo la kukuza
na kuendeleza sekta hiyo hapa nchini.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam juzi wakati wa hafla
ya kukabidhi vyeti kwa wanafunzi 25 wa UDSM waliohitimu Kozi ya Ukocha wa
Riadha Ngazi ya Kwanza inayotambuliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa
(IAAF), ‘IAAF Coach Level 1’, na Mkuu wa Idara ya Michezo na Viungo wa chuo
hicho, Dk. Steven Mabagala.
Dk. Mabagala, alisema Riadha wameonesha njia kwa kupata elimu
ambayo ni njia ya kufikia mafanikio yatakayoisaidia nchi.
Aidha, aliwataka wahitimu wa kozi hiyo, kuwafundisha watoto
mchezo wa riadha na kutoviweka kabatini vyeti hivyo na badala yake wavitumie
kwa maslahi ya mchezo huo.
"Kozi mliyoshiriki isiwe mwisho, bali mpanue wigo zaidi
ya mliyoyapata katika elimu inayotambulika na IAAF," alisema Dk. Mabagala.
Alipongeza kozi hiyo kwa kueleza kwamba, imetolewa wakati
muafaka na kuwataka wahitimu hao kuwafundisha watoto kwa sababu hiyo ni kozi ya
kitaaluma zaidi.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT),
Wilhelm Gidabuday, alisema elimu waliyoipata wanafunzi hao ni sehemu ya
historia kwa sababu ya unyeti wake.
Gidabuday, alisema sababu ya kuwa ni ya kihistoria ni kwa
sababu Mkufunzi aliyeitoa ni sahihi katika mchezo huo.
"Kozi inayotambuliwa na IAAF imempata mtu sahihi ambaye
ni Dk. Hamad Ndee, hakuna mwenye mashaka, lakini tunashangazwa kozi nyingi
zinazotolewa huko mitaani ambazo hata sisi RT hatuzijui zinatuchafulia mchezo
wetu," alisema Gidabuday.
Aidha, Gidabuday alisema wanafunzi hao wa mwaka wa pili
chuoni hapo, wamechagua kujifunza mchezo muhimu ambao ni mama wa michezo yote
na kuwataka kuongeza juhudi zaidi michezoni.
Mtendaji huyo, alitumia fursa hiyo kueleza kwamba idadi kubwa
ya Watanzania imeelekeza akili zao kwenye mbio ndefu na kuwasahau mashujaa walioiletea
nchi heshima katika upande mwingine wa riadha, ambako medali ya kwanza hapa
nchini ililetwa na mwanamke ambaye ni Theresia Dismas aliyetwaa medali ya fedha
mwaka 1965 katika mashindano ya Afrika yaliyofanyika Congo Brazzaville.
Naye Mkufunzi wa kozi ambaye anatambuliwa na IAAF, Dk. Ndee,
alisema hiyo ni kozi ya kwanza na ya aina yake hapa nchini, ambayo imeanzia
UDSM na baadaye itahamia mikoani.
Naye mmoja wa washiriki wa kozi hiyo, Said Mohamed, alisema mafunzo waliyoyapata watayafanyia
kazi na kueleza kuwa, sio mwisho wao bali wataendelea mbele zaidi.
No comments:
Post a Comment