WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi
wa mkoa wa Ruvuma uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo na kuondoa
vikwazo vyote ili kuvutia wawekezaji zaidi.
“Mkoa wa Ruvuma kama ilivyo mikoa mingine,
unazo fursa ambazo zikiendelezwa, zitaleta tija na kusaidia kuongeza kasi ya
ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Nitoe rai kwa mkoa uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo
sambamba na kuondoa vikwazo vyovyote vya uwekezaji na biashara ili kuvutia
zaidi wawekezaji wa ndani na nje,” amesema.
Ametoa wito huo leo mchana (Alhamisi,
Julai 25, 2019) wakati akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji mkoani
Ruvuma linaloendelea kwenye uwanja wa Majimaji, Manispaa ya Songea. Pia
amezindua Mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa huo.
Amesema katika ustawi wa uchumi, nchi nyingi hapa duniani
zimeweza kukuza uchumi wao kupitia ujenzi wa viwanda na zikafanikiwa kupunguza
umasikini katika jamii zao. Amezitaja nchi hizo kuwa ni Marekani, China,
Japani, Korea ya Kusini na Ujerumani.
“Tunapaswa kuiga kutoka wa wenzetu. Ndiyo maana Tanzania
pia tunahamasisha ujenzi wa viwanda kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mikoa ili
tulete mageuzi ya kiuchumi yatakayowezesha upatikanaji wa ajira na hatimaye
kuondoa umaskini,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza:
“Kongamano hili ambalo kaulimbiu yake ni “Ruvuma itavuma kwa uchumi wa viwanda,
wekeza sasa,” imelenga kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo mkoani
humu, na inajipambanua vema na kuendana
na azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na
viwanda ifikapo 2025.”
Amesema mchango wa sekta ya viwanda kiuchumi
na kijamii nchini ni pamoja na kuongeza pato la Taifa na kupandisha hali ya
maisha ya wananchi; kusaidia nchi isiyumbe kiuchumi ikizingatiwa kuwa viwanda
vingi havitegemei hali ya hewa kama kilimo; kuboresha urari wa biashara (improve balance of trade) kwa sababu
tija yake ni kubwa na hasa zikiuzwa bidhaa nyingi nje ya nchi na kupunguza
uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Amezitaja faida nyingine kuwa ni kuchangia
maendeleo ya sekta nyingine kama za kilimo, uvuvi, elimu na madini; kutengeneza
ajira kwa wananchi; kuchagiza na kuharakisha maendeleo ya teknolojia na
rasilimali watu na kuwezesha matumizi mazuri ya maliasili zilizopo kwa faida zaidi.
Nyingine ni kuleta uhakika wa soko la
mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini kwa sababu hutumika kama
malighafi na kuwepo kwa uhakika wa kuingiza fedha za kigeni nchini kupitia
mauzo ya bidhaa nje ambapo husaidia kuagiza mitambo, malighafi na bidhaa
nyingine ambazo hazizalishwi nchini.
Mapema, akitoa salamu kwa
niaba mabalozi wengine, Mwakilishi wa Balozi wa China, Bw.
Xian Ding alisema ana
uhakika kuwa kongamano hilo litafanikiwa kuleta mabadiliko mkoani humo kwa sababu wana bidii ya kazi.
“Ninaahidi kuleta wawekezaji kutoka China
kwa sababu tunataka waje kuleta teknolojia mpya, wafanye kazi pamoja na
Watanzania na wawafundishe teknolojia hizo mpya. Tunataka hapa Ruvuma iwe model
(mfano) kwa mikoa mingine,” alisema.
Akielezea
kwa
kifupi kuhusu mwongozo uliozinduliwa na Waziri Mkuu, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF),
Dkt. Hoseana Lunogelo alisema walitumia mfumo shirikishi ili kupata mwongozo
unahusisha wawekezaji wa ndani.
“Mwongozo huu umezingatia Dira ya Taifa
ya 2025 katika kutimiza azma ya Serikali ya kuwa nchi ya uchumi na viwanda,
tumeshirikisha wananchi wa mkoa wa Ruvuma ili wasibakie kuwa watazamaji,”
alisema.
No comments:
Post a Comment