HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 13, 2019

Rais Ramaphosa kuwasili nchini kesho

NA SULEIMAN MSUYA

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa atawasili nchi kesho kwa ziara ya kitaifa na kushiriki Mkutano wa 39 wa viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Aidha, Mabalozi 42 wa wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali leo watatembelea Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Jilius Nyerere (JNHPP) unaojengwa katika maporoko ya Mto Rufiji.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk.Hassan Abas wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Alisema Ramaphosa akuwa Rais wa kwanza kuwasili nchini ambapo leo atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake Rais John Magufuli na baadae ataendelea na ziara zake katika maeneo mengine.

Msemaji huyo alisema Rais Ramaphosa Agosti 16 Ijumaa atafanya ziara ya kutembelea eneo la Mazimbwi ambalo lina historia na nchi ya Afrika Kusini.

"Leo tutampokea Rais Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye anakuwa Rais wa kwanza kuwasili kwa ziara ya kikazi lakini pia mkutano wa 39 wa SADC utamkuta hapa," alisema.

Alisema uamuzi wa kiongozi huyo kuamua kutangulia ni ishara tosha kuwa Tanzania ni nchi ambayo inakubalika kwa nchi jirani na wanachama wa SADC.

Alisema wakati Rais Ramaphosa akiwa wa kwanza kuwasili nchini nchi zote 16 wanachama zimethibitisha kushiriki mkutano wa 39 wa SADC unaonza Agosti 17.

Kuhusu ziara ya mabalozi wa Tanzania kutembelea mradi wa JNHPP ni katika kuhakikisha wanaona na kutambua juhudi zinazofanywa na Serikali kupigania maendeleo.

Dk. Abas alisema mabalozi hao pamoja nakutembelea mradi huo watashiriki mkutano wa 39 wa SADC ili waweze kujua mikakati ya Uenyekiti mpya wa nchi yao.

Alisema kimfumo mabalozi hao ni wenyeviti wa SADC kwa mabalozi wa nchi za SADC wanazowakilisha hivyo ni haki yao kushiriki mkutano huo wa aina yake.

"Tunataka mabalozi wetu wapite waone Tanzania mpya ya Magufuli inavyofanya mambo makubwa na tunataka wakirudi huko walipo watuletee wawekezaji kwani ubalozi sasa unataka kufanyika kwa diplomasia ya uchumi," alisema.

Aidha, Msemaji huyo aliwataka Watanzania kushiriki kwenye kongamano litakalohutubiwa na Rais mstaafu wa awamu wa tatu Benjamin Mkapa.

Alisema Mkapa atatumia kongamano hilo kuelezea historia ya SADC, hivyo ni fursa yakipekee kwa Watanzania kujifunza.

"Kama unataka kupata uzoefu na uzeefu mtu sahihi ni Mzee Mkapa kwani ameanzia uandishi, uofisa, uwaziri hadi Rais anaijua sana SADC njooni mjifunze," alisema

No comments:

Post a Comment

Pages