SERIKALI ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) katika
kutatua changamoto zinazotokana na uwepo wa wakimbizi nchini pamoja na
kutafuta suluhu ya kudumu kwenye nchi zao ili wakimbizi hao waweze
kurejea makwao kuendelea na shughuli za maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo (Ijumaa, Agosti 30, 2019) katika mazungumzo yake na Kamishna Mkuu wa UNHCR, Bw. Filippo Grandikwenye
Kituo cha Maonyesho cha Yokohama nchini Japan baada ya kuhitimishwa kwa
Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 7).
Katika
mazungumzo hayo, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa UNHCR kuisaidia
mikoa inayokaliwa na wakambizi kutokana na kuharibiwa kwa mazingira.
“Hata hivyo Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na UNHCR
kuimarisha ulinzi wa maeneo ya wakimbizi ili wananchi wa maeneo hayo
waendelee kuishi kwa amani na utulivu.”
Kwa upande wake, Kamishna
Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Bw.
Filippo Grandi amesema amefurahishwa na utayari wa Serikali ya Tanzania
katika kupokea wakimbizi na usikivu wa Rais Dkt. John Magufuli katika
kushughulikia changamoto za wakimbizi.
Waziri
Mkuu yupo nchini Japan akimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye
Mkutano wa Kilele wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya
Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 7) ambao umehitimishwa leo.
Waziri
Mkuu ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya
Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na viongozi mbalimbali kutoka
Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment