Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimsikiliza Mkuu
wa Idara ya Ardhi na Maliasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Dustan
Kitandula (kushoto) alipokwenda kutangaza uamuzi wa Serikali kufuta Mashamba
matatu ya Mkomazi Plantantions Co Ltd maarufu MOA leo tarehe 30 Agosti 2019. (Picha na Wizara ya Ardhi).
Na Munir Shemweta, WANMM MKINGA
Serikali imefuta miliki
ya Mashamba matatu ya Mkomazi Plantantions maarufu MOA yaliyopo wilaya ya
Mkinga mkoani Tanga kutokana na kukiuka masharti ya uendelezaji ikiwemo kutelekezwa
bila kufanyiwa maendelezo yaliyokusudiwa
na kutolipiwa kodi ya pango la ardhi.
Uamuzi huo umetangazwa
leo tarehe 30 Agosti 2019 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
William Lukuvi alipozungumza na wananchi wa Mayomboni wilayani Mkinga mkoani
Tanga alipokwenda kutatua mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo.
Mashamba yaliyofutiwa
ni lenye hati Na 9780 na ukubwa wa ekari
14,688, shamba Na 4268 ekari 804 na Shamba lenye Hati Na 9781 ekari 246 ambapo mashamba yote matatu yana
ukubwa wa ekari 15,738.
Kufuatia uamuzi huo,
jumla ya vijiji kumi vyenye kaya 3,236 zilizo na wakazi 16,450 zitanufaika na
uamuzi wa serikali kutokana na wananchi wake kuvamia mashamba hayo na kufanya
maendelezo ya kujenga makazi, shule pamoja na kuendesha shughuli za kilimo cha
mazao ya kudumu na ya muda mfupi.
Vijiji vilivyonufaika
ni uamuzi wa Serikali kufuta mashamba ya Mkomazi Plantations ni kijiji cha Kilulu-Dunga,
Zingibari, Mwaboza, Mwakikoya, Mhandakini, Nkanyeni, Sigaya, Mayomboni,
Ndumbani pamona na kijiji cha Moa
Akizugumza wakati wa
kutangaza uamuzi huo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William
Lukuvi amesema uamuzi wa kufuta mashamba hayo matatu unafuatia maombi
yaliyotumwa kwa Raisi John Pombe Magufuli ya kutaka kufutwa mashamba hayo kutokana
na kutoendelezwa na wamiliki wake kwa muda mrefu.
Alisema, Rais ameridhia
maombi hayo kwa kuwa serikali imekuwa ikisisitiza utekelezwaji wa sheria ya
Ardhi Na 4 ya mwaka 1999 ikiwemo uendelezaji wa mashamba ambayo yamemilikishwa
sehemu mbalimbali nchini.
Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi aliagiza kufanyika upimaji katika vijiji vyote kumi
vilivyopo ndani ya shamba hilo sambamba na kuanishwa miapaka ya vijiji hivyo na
kupatiwa hati ambapo alitaka wananchi wanaishi kwenye vijiji hivyo kutobughudhiwa.
Aidha, Waziri Lukuvi alitaka
maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya uwekezaji katika shamba yaliyofutwa kuachwa kwa
ajili ya shughuli hiyo ikiwemo muwekezaji wa Katani Azka International Tanzania
mwenye ekari mia tano pamoja na maeneo ya viwanda kama kile cha kuzalisha
chumvi na kusisitiza kuwa serikali inataka uwekezaji utakaotoa ajira kwa vijana
na wakati huo kupata mapato kupitia kodi ya pango la ardhi.
Katika
hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi ameagiza kufanyika uhakiki wa mashamba mengine ya Kwa
Mtili Estates Co Ltd yaliyopo Mkinga mkoani Tanga ambapo ekari 58 pekee ndizo
zilizoombwa kufutwa kwa Rais kutokana na kutoendelezwa huku mmili wake ikidaiwa
kumiliki ekari 2,841.
Hatua hiyo inafuatia
Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili katika halmashauri ya wilaya ya Mkainga Obed
Katonge kueleza kuwa, Kwa Mtili Estates Co Ltd inalo shamba la lenye ukubwa wa
ekari 2,841 tofauti na inavyoonekana katika kumbukumbu za ofisi ya Msajili wa
Hati Kanda ya Kaskazini ambazo ni 58.
Lukuvi aliagiza
wataalamu wa ardhi kutoka Kanda ya Kaskazini kufanya uhakiki huo katika kipindi
cha mwezi mmoja na kumpa taarifa ya uhakiki huo mwisho wa mwezi Septemba 2019 na
kufafanua kuwa pale itakapothibitika kuna ujannja uliofanyika wa kumuongeza
mmiliki wa shamba hilo hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Mbunge wa Jimbo la
Mkinga mkoani Tanga Dustan Kitandula aliishukuru serikali ya awamu ya tano kwa
kusikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wanaoishi eneo la shamba
lililofutwa la kutaka kurejeshewa ardhi yao waliyokuwa wakiutumia kwa shughuli
mbalimbali.
Alisema, mgogoro wa
ardhi baina ya wananchi wa mkinga na wamiliki wa mashamba ya Mkomazi
Plantantions Co Ltd umekaa kwa muda mrefu na kuwafanya wananchi kuwa na ndoto
isiyokuwa na majibu lakini uamuzi uliotolewa na Serikali umewafanya kuishi kwa
furaha na amani .
No comments:
Post a Comment