WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema changamoto ya barabara ya kutoka Ifakara
hadi Mlimba iliyokuwa inawakabili wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu
imepatiwa ufumbuzi baada ya Serikali kupanga kuijenga kwa kiwango cha
lami.
Amesema
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli
imedhamiria kuboresha miundombinu ya barabara nchini ikiwemo barabara ya
kutoka Ifakara hadi Mlimba yenye urefu wa km. 126.5.
Waziri
Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumapili, Septemba 15, 2019) wakati
akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
uwanja wa Matangini, Mlimba wilayani Kilombero.
“Serikali
imedhamiria kuimarisha barabara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa
ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Ifakara-Mlimba kwa kiwango cha lami
lengo likiwa ni kurahisisha usafiri pamoja na kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.”
Alisema
Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo kwa ajili ya kuboresha
maendeleo ya wananchi na kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, hivyo
aliwataka wananchi hao waendelee kuiamini Serikali yao.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu alimuagiza Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Morogoro, Jackson
Mpankuli ahakikishe amepeleka walimu katika shule ya msingi Matangini na Mwangazaambazo zinakabiliwa na upungufu wa walimu.
Waziri
Mkuu alisema hadi Sepetemba 30 mwaka huu kiongozi huyo awe
ameshawahashimia walimu katika shule husika. Waziri Mkuu alitoa agizo
hilo baada ya Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Suzan Kiwanga kulalamikia
upungufu wa walimu hao.
Mbunge
huyo alisema katika jimbo kuna tatizo kubwa la upungufu wa walimu hali
inayosababisha baadhi ya wazazi kukodi walimu kwa ajili ya kuwafundisha
watoto wao, hivyo Waziri Mkuu aliagiza walimu wahamishiwe katika shule
ndani ya wiki mbili.
Akizungumza
na wananchi katika eneo la Mchombe alipokuwa njiani kuelekea Mlimba,
Waziri Mkuu aliwataka wazazi, walezi na viongozi wa halmashauri ya
wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kuhakikisha wanadhibiti ongezeko la
mimba kwa watoto wa shule.
“Lazima
kuwalinda watoto wa kike ili wasipate mimba kwani watashindwa kuendelee
na masomo, hivyo watashindwa kutimiza ndoto zao. Viongozi simamieni
utekelezaji wa sheria kwa kuwachukulia hatua wote waliowapa mimba
wanafunzi.”
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, Mbunge wa jimbo la Kilombero, Lijualikali na
Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga waliiomba Serikali iwasaidie ujenzi wa
barabara za kutoka Ifakara hadi Mlimba na barabara ya Ifakara hadi
Kidatu ambayo ujenzi wake unasuasua.
Pia Suzan alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa
kutenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa barabara ya
Ifakara-Mlimba na baadae kuwekwa lami kwa awamu na kusema kuwa Serikali
ya Awamu ya Tano ikiahidi kitu inatekeleza
Waziri
Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro ambapo
anatarajiwa kutembelea Halmashauri za wilaya ya Ulanga na Malinyi
kukagua miradi ya maendeleo ukiwemo mradi wa ujenzi wa hospitali ya
wilaya na kuzungumza na wananchi pamoja na watumishi.
No comments:
Post a Comment