WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema zaidi ya vijana 46,000 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya stadi za kazi kwa njia ya uanagenzi kupitia taasisi ya Don Bosco Net Tanzaniakatika mwaka huu wa fedha.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 14, 2019) wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo na maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Kazi Duniani (ILO), katika viwanja vya Donbosco jijini Dodoma.
“Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, imeandaa
Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini ambayo imelenga kutoa mafunzo ya stadi
mbalimbali za kazi kwa vijana wa ngazi mbalimbali za elimu kuanzia
wahitimu wa darasa la saba hadi vyuo vikuu.”
Waziri
Mkuu amesema miongoni mwa mafunzo yanayotolewa chini ya programu hiyo
ni ya uanagenzi (apprenticeship) ambayo yalianza 2017 na 2018 walihitimu
vijana 32,786.
Waziri Mkuu amesema katika awamu ya pili ya mafunzo hayo yaliyozinduliwa leo ambayo yanahusisha jumla ya vijana 5,875kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 ya ILO.
Amesema
licha ya mafanikio yaliyoonekana katika sekta ya Kazi na Ajira kwa
kipindi cha miaka 100 iliyopita, suala la ukosefu wa ajira kwa vijana ni
miongoni mwa changamoto inayoikabili dunia, hivyo linahitaji kuwekewa
mikakati endelevu kwa miaka 100 ijayo.
Waziri Mkuu amesema miongoni
mwa sababu zinazotajwa kuchangia ukosefu wa ajira kwa vijana ni vijana
kutokuwa na ujuzi sahihi wa kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa katika
sekta mbalimbali za kiuchumi.
Kwa upande wake,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Wenye
Ulemavu, Jenista Mhagama amesema hadi kufikia Juni 2019 jumla ya vijana
36,726 wamefaidika na programu ya kukuza ujuzi inayogharamiwa na
Serikali wa asilimia 100.
Amesema
kati yao vijana 6,455 walinufaika na mafunzo ya uanagenzi katika fani
mbalimbali zikiwemo za ushonaji na nguo, useremara, uashi, terazo,
uchongaji wa vipuri, ufundi magari, umeme na utengenezaji wa viatu vya
ngozi.
Waziri
huyo amesema mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo
rasmi wa mafunzo yametolewa kwa vijana 10,443 katika fani za uashi,
useremara, ufundi wa magari, upishi na huduma za hoteli.
Pia,
Waziri Jenista amesema kwa upande wa mafunzo ya kilimo cha kisasa jumla
ya vijana 18,800 walinufaika na mafunzo hayo huku vijana wengine 1,028
walipatiwa mafunzo ya vitendo pahala pa kazi.
Naye,
Mratibu wa Miradi wa Taasisi ya Donbosco Tanzania, Rosemary Terry Njoki
amesema programu ya kukuza ujuzi imezingatia kuwawezesha vijana wa
miaka kati 17 hadi 35 kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au
kuajiriwa.
Amesema
mafunzo hayo yataliwezesha Taifa kufikia lengo lake ya kukuza uchumi
kutoka wa chini kwenda wa kati ifikapo 2025 kwa kuwa yatakuwa yameongeza
wafanyakazi wenye ujuzi ambao wanahitajika kwa wingi.
Awali, Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki, Wellington Chibebe amesema shirika hilo limedhamiria kupigania haki ya kijamii pamoja na haki za binadamu na kazi zinazotambulika kimataifa.
Amesema
tangu mwaka 1919, ILO ni shirika pekee la Umoja wa Mataifa lenye mfumo
wa utatu unaowaleta pamoja wafanyakazi, waajiri na Serikali katika nchi
187 wanachama wa shirika hilo katika kuweka viwango vya masuala ya kazi,
kukuza sera na kupanga programu za zinazochagiza kazi zenye staha kwa
watu wa jinsia zote.
“Maadhimisho
ya karne moja ya ILO ni fursa nzuri ya kujitathimini wapi lilipotoka,
kusheherekea historia na mafanikio yake na pia kutafakari siku zijazo.
Pia ni jukwaa la kipekee la kuihakikishia dunia umuhimu wa jukumu na
mamlaka yake ya kutetea haki ya kijamii na ajenda ya kazi zenye staha”
Baada
ya uzinduzi huo, Waziri Mkuu alishiriki shughuli ya kupanda jumla ya
miti 200 katika Mji wa Serikali, Mtumba kuashiria miaka 100 ya ILO
iliyopita na miaka 100 ijayo.
No comments:
Post a Comment