HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 17, 2019

Wakurugenzi waagizwa kuwafuatilia walengwa wa TASAF

 Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk. Dorothy Gwajima , akizungumza na Mtendaji wa Kata ya Msoga mkoa wa Pwani, Tegemeo Mtahondi mbele ya mnufaika wa TASAF, Fatma Sheria (aliyejifunika kanga), huku Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akishuhudia. Viongozi hao walimtembelea Sheria aliyejenga nyumba ya bati baada ya kuingia kwenye mpango wa TASAF.
 
NA MWANDISHI WETU, PWANI

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dk. Dorothy Gwajima, amewataka Wakurugenzi wote nchini kuhakikisha kila idara inafuatilia  na kutoa ripoti ya maendeleo ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini zaidi (TASAF) kwenye idara zao.

Akizungumza wakati wa kikao cha wakuu wa idara na Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Teresia Mmbamdo, Dk. Gwajima alisema TASAF ni lazima kila idara itekeleze mpango huu badala ya kuwaachia waratibu na wafuatiliaji.

"TASAF ni mpango wa kila idara nchi nzima hivyo basi nawaagiza Wakurugenzi wote kufuatilia kwa kuwatambua na kuwatembelea walengwa sio mnawaacha tu.

"Kushindwa kwa mpango huu ni kushindwa kwetu kuanzia mtendaji wa chini hadi juu lakini pia kushindwa ni kwenda kinyume cha azma ya Rais John Magufuli mimi sitaki hilo litokee," alisema Dk. Gwajima.

Alisema walengwa wa TASAF, wanafanya shughuli za kilimo, ufugaji, afya na miradi ya miundombinu hivyo wanatakiwa kufuatiliwa na taarifa za ziwekwe kwa utaratibu maalum wa kufahamika.

Alisema lazima mambo mengi mazuri ya maendeleo yanayofanywa na walengwa wa TASAF yatangazwe ili hata wachache wasio fahamu kuhusu mpango huu waone na kulewa.

"Umaskini ni dhana hivyo Serikali hii imeamua kuleta mbegu kwa hao wanaoitwa maskini wanapewa elimu sahihi ya matumizi ya fedha namna ya kuunda vikundi, kuweka akiba na kukopa ndio maana walengwa wa TASAF waliokuwa wanaishi kwenye tembe sasa wanalala katika nyumba za bati, wanalima na kufuga wapo vizuri," alisema.

Dk. Gwajima ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi TASAF taifa, alisema lazima haki za walengwa wa mpango huo zilindwe kwa kuwa wamechaguliwa kwa uwazi bila kujali dini, kabila wala chama.

Kabla ya kuahirishwa kwa mkutano huo, Mmbamdo alisema Mkoa wa Pwani unakabiliwa na changamoto ya chumba cha kuhifadhi maiti.

"Zinapotokea ajali vibaka wanawaibia majeruhi na marehemu vitu vyao hadi kadi za matibabu hivyo wengine kushindwa kutibiwa na maiti kukosa ndugu matokeo yake halmashauri inawazika.

"Chumba cha maiti hapa Tumbi ni kidogo naomba ulipokee hili na kulifanyia kazi," alisisitiza Mmbando.

No comments:

Post a Comment

Pages