WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa ameiomba Serikali ya Japan ikubali kutoa mafunzo
zaidi kwa Madaktari Bingwa wa upasuaji (Nephrologist Surgeon
Specialist) na Madaktari Bingwa (Nephrologist Physician Specialist) wa
magonjwa ya figo na moyo kutoka Tanzania ili kukidhi mahitaji makubwa ya
madaktari hao nchini.
Waziri
Mkuu amewasilisha ombi hilo jana jioni (Septemba, 02, 2019) wakati
alipozungumza na Mshauri Maalum wa Masuala ya Afya wa Taasisi ya
Tokushukai General Incorporated Association iliyo chini ya Serikali ya
Japan, Bw. Akio Egawa kwenye uwanja wa ndege wa Narita nchini Japan
akiwa njiani kurejea nyumbani.
Waziri
Mkuu alisema hivi sasa Tanzania ni kimbilio kwa nchi jirani katika tiba
ya moyo na figo, hivyo Madaktari Bingwa wa Upasuaji na Madaktari Bingwa
wa magonjwa hayo wanahitajika sana.
Alisema
baada ya hospitali ya Benjamini Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma
kufanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa saba chini ya ufadhili wa
Taasisi hiyo, nchi jirani pia zinategemea kupata huduma hiyo nchini
Tanzania, hivyo madaktari na vifaa tiba zaidi vinahitajika Ili kujenga
uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wa ndani na nje.
Waziri
Mkuu aliishukuru Serikali ya Japan kupitia Taasisi hiyo kwa misaada
yake ambayo kwa kiwango kikubwa imefanikisha kuanzishwa kwa tiba ya
upandikizaji figo katika hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha
Dodoma.
“Nashauri
uandaliwe utaratibu wa kubadilishana watalaam ili Watanzania waende
Japan kutibu wagonjwa na Wajapan waje nchini kufanya kazi kwenye
hospitali zetu lengo likiwa ni kubadilishana ujuzi na kuongeza
uzoefu.”
Pia,
Waziri Mkuu alimkaribisha nchini Tanzania Bw. Egawa ili aweze kuona
mwenyewe maeneo mengine ambayo Taasisi anayoiongoza inaweza kusaidia
ili kuifanya nchi yetu kuwa na uwezo mkubwa katika tiba ya uapandikizaji
wa figo Barani Afrika.
Waziri
Mkuu alisema amefurahi kufahamu kuwa Bw. Egawa ameishi Tanzania kwa
miaka mitatu akifanya kazi kwenye ubalozi wa Japan uliopo Dar es
Salaam, hivyo anaifahamu vizuri Tanzania na anajua umuhimu na mahitaji
ya huduma za afya nchini na anafahamu mikakati Serikali kuhusu kuboresha
huduma za afya.
Kwa upande wake,
Bw. Egawa alimwahidi Waziri Mkuu kuwa Taasisi yake iko tayari kuunga
mkono juhudi za Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt.
John Magufuli kwa kuendelea kusaidia hospitali ya Benjamin Mkapa ili
kuiimarisha na kuiwezesha kufanya vizuri zaidi katika huduma ya tiba ya
figo na moyo. Alisema taasisi yake iko tayari kuendelea kutoa
ushirikiano na Serikali ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment