Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), DK. Agnes Kijazi, akizungumza katika warsha ya waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba iliyofanyika Septemba 2, 2019 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri, Samwel Mbuya na kulia ni Mkurugenzi Huduma za Utabiri, Dk. Hamza Kabelwa. (Picha na Francis Dande).
Mkurugenzi Huduma za Utabiri, Dk. Hamza Kabelwa, akifafanua jambo wakati akizungumza katika warsha hiyo.
Mtabiri wa Hali ya Hewa, Abubakar Lungo, akitoa mada kuhusu mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli, Oktoba hadi Disemba 2019.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi, amewataka wanahabari kuhakikisha taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinawafikia walengwa kwa haraka na usahihi zaidi.
Kijazi aliyasema hayo Septemba 2, 2019 wakati akifungua warsha ya wanahabari kuhusu mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kwa kipindi cha mwezi Octoba hadi Disemba mwaka huu, iliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo uliopo Ubungo Plaza jijini Dar Es Salaam.
Alisema kuwa warsha hiyo ni juhudi za mamlaka kuhakikisha taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinawafikia walengwa ikiwemo jamii kwa uhakika na usahihi Zaidi, ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na pia kusaidia mamlaka zinazohusika kupanga mipango ya kukabiliana majanga yatakayo na hali mbaya ya hewa.
“lakini kwa kipekee naamini warsha hii itakuwa na tija Zaidi kwa vile hivi karibuni kumekuwa na changamoto mbalimbali za hali mbaya ya hewa kama vile upepo mkali uliopelekea kusimamishwa kwa huduma za usafiri baharini, mvua kubwa zilizosababishwa wananchi kukosa makazi, joto kali lililozua taharuki kwa wakazi wa Pwani na Kaskazini, nikiwa kama kiunganishi cha TMA na wananchi tunaomba na kuzidi kusisitiza umuhimu wa kusambaza taarifa za hali ya hewa zinazotolewa kwa umakini” Amesema Kijazi.
“Serikali ya awamu ya tano inatambua vyema mchango mkubwa wa huduma za hali ya hewa nchini na umuhimu wa kuwafikia wananchi wote kwa wakati. Hivyo basi ili kudhihirisha hilo Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini imekuwa ikahakikisha inakutana na wanahabari ambao ni daraja muhimu kati ya taasisi zetu za serikali na wananchi wote kwa ujumla”.
“Vilevile kutokana na maoni ya wanahabari na wadau wengine kuhusu lugha inayotumika kuwasilisha taarifa za hali ya hewa kuwa wakati mwingine imesheheni maneno ya kisayansi na yasiyo rahisi kueleweka na jamii, mamlaka kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na taasisi zingine ikiwemo BAKIZA na vyuo vikuu, imeweza kufafsiri baadhi ya maneno kwa lugha ya Kiswahili. Kupitia warsha hii, wanahabari mtapata fursa ya kuona baadhi ya misamiati ya hali ya hewa iliyo katika lugha ya Kiswahili kwaajili ya kutoa maoni yenu kabla haijaanza kutumika rasmi” ameongeza Kijazi.
Aidha Kijazi amewataka wanahabari kuwa mabalozi wazuri wa TMA na umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa jamii katika shughuli za kila siku, pia aliwashukuru wanahabari kwa kuonesha ushirikiano wakati wa mkutano mkubwa wa 53, wa maandalizi ya utabiri wa mvua za vuli kwa nchi za Pembe ya Afrika (GHACOF 53), uliofanyika hapa nchini Agosti 26-28 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment