HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 03, 2019

DKT. KIJAJI AITAKA TRA KUONGEZA WIGO WA WALIPA KODI

Na Ramadhani Kissimba, WFM, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kuandaa Mkakati mahsusi utakaosaidia kuongeza wigo wa walipa kodi nchini kutoka idadi ya walipa kodi elfu mbili waliopo sasa.

Dkt. Kijaji aliyasema hayo alipofanya ziara ya kawaida ili kukagua utendaji kazi wa Mamlaka hiyo katika Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ya Mkoa wa kikodi wa Kinondoni.

Mhe.Naibu Waziri alisema ili kuwaondolea mzigo walipa kodi waliopo sasa, jitihada za makusudi zinahitajika ili kuongeza idadi ya walipa kodi.

Dkt. Kijaji ameitaka TRA kuandaa mpango mkakati utakaoonyesha kuwa baada ya miaka miwili Mamlaka hiyo itakuwa imeongeza idadi ya walipa kodi zaidi ya milioni mbili,kwa kufanya hivyo Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania watakuwa wamejibu hoja iliyotolewa na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwaondolea mzigo walipa kodi waliopo sasa.

Aidha Mhe. Kijaji ameitaka TRA kumuandalia na kuwasilisha kwake takwimu ya ongezeko la walipa kodi lililotokana na zoezi la kugawa vitambulisho vya wajasiriamali nchini.

“Lengo la kugawa vitambulisho hivyo lilikuwa ni kuongeza wigo wa walipa kodi, hivyo ni vyema kujua tumeongeza walipa kodi wangapi waliotokana na zoezi hilo” alisisitiza Dkt. Kijaji

Kwa upande wa kodi ya majengo, Dkt. Kijaji ameitaka Mamalaka ya Mapato Tanzania kuhakikisha inapata orodha ya nyumba zote nchini kwa kuorodhesha wamiliki wa nyumba hizo na mawasiliano yao na kisha kuandaa kanzi data itakayosaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi hiyo.

Dkt. Kijaji amesema ili kudhibiti upotevu mapato yanayotokana na kodi ya majengo ni lazima TRA wafanye kazi usiku na mchana kuhakikisha kanzidata ‘database’ hiyo inakamilika ambayo itatumika kuwakumbusha walipa kodi kupitia ujumbe mfupi wa simu ambapo itasaidia katika ukusanyaji wa kodi hiyo.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Meneja wa Mkoa wa kodi wa Kinondoni Bw. Massawe Masatu alisema kuwa pamoja na changamoto wanazopitia, Ofisi ya Mkoa wa kodi wa Kinondoni kwa mwaka 2018/19 ilikusanya zaidi ya shilingi bilioni 713ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 794, sawa na asilimia 86 ya lengo.

Mhe. Naibu Waziri aliwapongeza watumishi wa Mamlaka hiyo na kuwataka kuwatumia vizuri watumishi hao katika kuongeza mapato ili kuwezesha Serikali kuwahudumia vyema wananchi.

Dkt. Kijaji ameuagiza Uongozi wa Mamlaka hiyo kuwapa ushirikiano watumishi wanaofanya kazi zao kwa weledi, na kutosita kuwachukulia hatua wale wote watakaonekana wana nia ya kuirudisha nyuma Mamlaka hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages