Maofisa Mawasiliano wa Wizara mbalimbali zinazohusika na rasilimali misitu wakiwa na maofisa wa Shirika Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG) baada ya kumaliza mkutano wao mkoani Morogoro.
NA SULEIMAN MSUYA, ALIYEKUWA MOROGORO
SERIKALI imeshauriwa kuhamasisha jamii kuhifadhi misitu ya vijiji ili miradi maendeleo inayohitaji maji kuwa endelevu.
Ushauri
huo umetolewa na Meneja Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa
Tanzania (TTCS), Charles Leonard wakati wa mkutano wa siku moja wa
maofisa Mawasiliano wa Wizara zinazohusiana na misitu uliofanyika mkoani
Morogoro.
Leonard
alisema TTCS chini ya usimamizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili
Tanzania (TFGC), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania
(Mjumita) na Shirika la Kuendeleza Nishati Asili Tanzania (TaTEDO),
wamekuwa wakihamasisha uhifadhi endelevu wa misitu hivyo serikali
inapaswa kuongeza nguvu.
Alisema
mradi wa TTCS umeweza kushirikiana na wanavijiji wa vijiji 30 katika
wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro kuhifadhi misitu kwa mfumo
endelevu na matokeo yake yamekuwa chanya.
Meneja
huyo alisema miradi mikubwa kama ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa
Julius Nyerere (JNHPP) utaweza kuwa endelevu iwapo uhifadhi na utunzaji
wa misitu hasa ya vijiji utakuwa endelevu na shiririkishi.
"Niseme
wazi kuwa mradi kama JNHPP hauwezi kuwa endelevu iwapo misitu itaisha
na njia ya kuifanya iwe endelevu ni serikali kushirikiana na sisi na
wanavijiji ili kuitunza misitu ya vijiji ambayo ni asilimia 45 ya misitu
yote kwa endelevu," alisema.
Leonard
alisema mradi wa TTCS tangu kuanza kwake mwaka 2012 umewezesha
kuingizia vijiji na wanavijiji zaidi ya Sh.Bil.3 na uhifadhi kuimarika.
Alisema
mradi huo ambao unafikia ukomo mwezi Novemba mwaka huu umeweza
kuboresha huduma za kijamii kama elimu, afya, miundombinu, kilimo na
uchumi.
Akitoa mada
katika mkutano huo Ofisa Uhusiano wa TFCG, Bettie Luwuge alisema
wamekutana na maofisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Nishati, Mazingira, Kilimo, Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) na wadau mbalimbali ili kuwa na kauli moja kuhusu uhifadhi.
Luwuge
alisema kupitia maofisa mawasiliano hao ni wazi jamii itapata taarifa
kwa haraka kuhusu utunzaji na uhifadhi misitu kwa dhana ya uendelevu.
"Wananchi
ndio mlinzi mkubwa katika utunzaji wa misitu hivyo inatakiwa kunufaika
na rasilimali hiyo ili iweze kutunza kiundelevu," alisema.
Ofisa
huyo aliwataka maofisa hao kutumia nafasi zao kuwashawishi viongozi wa
wizara zao kuunga mkono jitihada hizo za uhifadhi endelevu.
Kwa
upande wao maofisa mawasiliano Issa Sabuni, Jaina Msuya, Mathew Kwembe,
Sophia Masuka, Rachel Lugoe walisema wadau hao wanapaswa kuungwa mkono
kwa kuongeza juhudi za kutoa elimu.
Walisema
mikakati ijikite kwenye utumiaji wa mitandao ya kijamii na vyombo vya
habari vya vilivyopo vijijini kuelimisha jamii kuhusu dhana nzima ya
utunzaji wa misitu.
No comments:
Post a Comment