HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 20, 2019

Watanzania Wahimizwa Kuzijua Haki Zao za Kisheria, Sio Kusubiri Mpaka Wapate Matatizo ya Kisheria Ndipo Waanze Kuhangaika

Watanzania, wamehimizwa kujitokeza kwa wingi katika mikoa yote ili kuzijua haki zao za kisheria, katika kila jambo, na sio kusuburi hadi kunapojitokeza matatizo yanahitaji ufumbuzi wa kisheria, ndipo wanahangaika kutafuta mawakili, na wengi kujikuta wanashindwa kumudu gharama za mawakili hivyo kupoteza haki zao, bila kujua uwepo wa msaada wa kisheria. 

Wito huo umetolewa leo mjini Bariadi Mkoani Simiyu, na Msajili wa watoa huduma za msaada wa kisheria, toka Wizara Katiba na Sheria, Bi Felister Joseph Mushi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho yam waka huu ya Wiki ya Msadda wa Kisheria, itakayo andishishwa kitaifa wilayani Bariadi, Mkoani Simiyu sambamba na maadhimisho kama hayo katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Bibi Mushi amesema, wananchi wengi wa kawaida hawazijui haki zao, na wengi huwa hawajishughulishi kuzijua haki zao, mpaka pale wanapopata matatizo ya kisheria, hivyo amewasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuhudhuria maadhimisho hayo ili kupata elimu ya ufahamu wa jinsi ya kupata msaada wa kisheria, pale wanapokumbwa na matatizo ya kisheria na sio kusubiri tatizo litokee ndipo wahangaikie ufumbuzi.

Bibi Mushi amesema lengo la maadhimisho hayo  yenye kauli mbiu ya  ”Msaada wa Kisheria kwa Maendeleo Endelevu”,  ni kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi, ila maadhimisho ya mwaka huu hayataishia katika utoaji tuu wa elimu kwa umma, bali yatakwenda sambamba na utoaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kisheria kwa watendaji wa ngazi mbalimbali na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, wasio na uwezo wa kumudu gharama za mawakili wa kujitegemea, zikiwemo huduma za bure kwa mahabusu na wafungwa magerezani.

Akizungumzia maandimisho yam waka huu kitaifa mjini Bariadi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya wa Bariadi, Melkzedeck Humbi, amesema maandimisho hayo ni muhimu sana kwa mkoa wa Simiyu, kwa sababu Mkoa wa Simiyu unaendeshwa kwa agenda ya maendeleo, hivyo kunapojitokeza matatizo yoyote ya kisheria, yanapunguza kasi ya utekelezaji wa agenda hivyo kwa kuutumia muda mwingi kusuluhisha migogoro badala ya kuleta maendeleo.

Mkurugenzi wa taasisi ya Mhola ya Kagera inayotoa msaada wa kisheria, Saulo Malauri, amesema taasisi yake imekuja kujiunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika jukumu zima la kuwapatia misaada ya kisheria kwa wananchi wasio na uwezo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa msaada wa kisheria, Christina Kamili Ruhinda, TANLAP, amesema shirika lake lina ratibu mashirika 78 ya msaada wa kisheria, hivyo wameungana na serikali kuhakikisha watu wasio na uwezo wa kumudu gharama za mawakili, wanapatiwa msaada wa kisheria bure ili wasipoteze haki zao kwa ukosefu tuu wa fedha za kumlipa wakili.

Mwanasheria Berious Nyasebwa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, amesisitiza kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo ”Msaada wa Kisheria kwa Maendeleo Endelevu” akisisitiza maendeleo endelevu yatapatikana pale tuu watu wote wenye hali zote, watapata haki zao za kisheria bila kujali wana uwezo wa kuajiri wakili au hawana. 

Maadhimisho haya, yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku ya Jumatatu, October 21 hadi Ijumaa October 25, 2019 Katika viwanja vya Halmashauri ya Bariadi na mikoani kote.

No comments:

Post a Comment

Pages