Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George
H. Mkuchika (Mb) akifafanua masuala ya kiutumishi kwa watumishi wa Sekretarieti
ya Mkoa wa Ruvuma na Halmashauri ya Wilaya ya Songea (hawapo pichani) wakati wa
kikao kazi chake kilichofanyika mjini Songea kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji
kwa watumishi hao.
Baadhi ya watumishi wa
Sekretarieti ya Mkoa wa Ruvuma na Halmashauri ya Wilaya ya Songea wakimsikiliza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wakati wa kikao kazi chake
kilichofanyika mjini Songea kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George
H. Mkuchika (Mb) akikabidhi msaada wa fedha taslimu na mahitaji kwa mlezi wa
kituo cha Swako cha kulea watoto yatima, Bi. Regina Chinguku kilichopo Songea
mkoani Ruvuma kwa niaba ya watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
waliochanga ili kukisaidia kituo hicho.
Na James Mwanamyoto, Songea
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt.
(Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amewapongeza Watumishi wa Umma wa Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kutoa msaada wa fedha, sabuni za kufulia na mafuta
ya kula kwa watoto yatima wa kituo cha Swako kilichopo Songea mjini kwani
wameonyesha taswira nzuri ya utumishi wa umma kwa wananchi ambao ndio walengwa
wakuu wa huduma zitolewazo na taasisi za Serikali.
Mhe. Mkuchika ametoa pongezi hizo
alipokutana na Watumishi wa Umma kwenye ziara yake ya kikazi yenye lengo la
kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kukagua
utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani humo.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya watumishi
hao, Mhe. Mkuchika amewashukuru watumishi waliochanga fedha hizo na kutoa mahitaji
mengine ambayo yamekuwa ni faraja kwa watoto hao.
“Msaada mlioutoa utakuwa ni chachu ya
kujenga ustawi wa watoto hao ili hapo baadae waweze kuwa na mchango katika
maendeleo ya taifa, na ndio maana mmemuona mlezi wa kituo hicho amefurahi sana
baada ya kupokea msaada wenu”, Mhe. Mkuchika amesisitiza.
Msaada
walioutoa watumishi hao ni mwendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ya
kuzitaka taasisi za umma nchini kuadhimisha
Wiki ya Utumishi wa umma mwaka huu kwa kushiriki masuala ya kijamii ili kujenga
uhusiano mzuri na wananchi.
Aidha, Mhe. Mkuchika amemshukuru Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Prof. Riziki
Shemdoe kwa kuratibu vema utekelezaji wa maelekezo ya ofisi yake katika
kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu kwani pamoja na kutekeleza
maagizo mengine wakati wa wiki hiyo ambayo huadhimishwa tarehe 16 hadi 23 Juni
kila mwaka lakini waliona pia ni vema wakawasilisha msaada kwa watoto yatima .
Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Prof. Riziki
Shemdoe alimueleza Mhe. Mkuchika namna watumishi wa Sekrekarieti ya Mkoa wa
Ruvuma walivyojitoa kuchanga fedha hizo na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu shughuli
za ustawi wa kijamii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Maadhimisho ya Wiki ya
Utumishi wa Umma nchini.
Mhe. Mkuchika anaendelea na ziara ya kikazi
mkoani Ruvuma yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, ikiwa
ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani
humo.
No comments:
Post a Comment