Jengo la Shule ya Sekondari Tabora Wavulana.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tabora Wavulana, shule hiyo alisoma Mwalimu Nyerere.
Na Irene Mark
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikishirikiana na baadhi ya wanahabari imedhamiria kuenzi, kutunza na kuiendeleza historia ya Mwalimu Julius Nyerere kwa kutembelea shule alizosoma na kufundisha hapa nchini.
Katika utekelezaji wa dhamira hiyo, imeandaa ziara ya kuona kazi za hayati Mwalimu Nyerere alizozifanya kwenye sekta ya elimu wakati taifa likiadhimisha miaka 20 baada ya kifo chake.
Akizungumza na waandishi wa habari waliopo kwenye ziara hiyo, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sylvia Lupembe alisema lengo ni kuhakikisha safari ya Mwalimu Nyerere kwenye elimu inafahamika na kuenziwa.
"Mwalimu alitoka kwenye familia ya chifu wote tunafahamu... hivyo alibahatika kupata elimu sawa na watoto wengine wa machifu enzi hizo lakini akawa wa tofauti kwa kutaka usawa yaani ubaguzi wa watoto wa machifu, wazungu na watoto kutoka familia za kawaida uondoke.
"Alitumia elimu aliyoipata kuisaidia Tanganyika kupata uhuru wake mwaka 1961 akaona haitoshi akasaidia sana kufanyika kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar leo tunajivunia Tanzania.
"...Kwa kuliona hili Wizara ya Elimi, Sayansi na Teknolojia ikaona ni vema kuadhimisha miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Nyerere na kinara wa ukombozi wa Tanganyika na baadhi ya nchi za Afrika kwa kutembelea maeneo ya kielimu aliyopita hapa nchini, hatuwezi kwenda nje ya nchi sisi tutaangalia alichokifanya akiwa hapa ili vizazi vijavyo visipoteze historia hii," alisema Lupembe.
Aliyataja baadhi ya maeneo yatakayotembelewa kuwa ni shule ya msingi Mwisengi alikoanzia Safari yake ya kielimu, shule ya sekondari Tabora, shule ya sekondari Mihayo zamani iliitwa St. Mary's ambako Mwalimu Nyerere ndipo alipoanzia kazi ya ualimu baada ya kutoka masomoni Uganda kwenye Chuo cha Makerere.
Maeneo mengine ni shule ya sekondari Pugu alikofanyia kazi kabla ya kuacha ualimu na kuelekeza nguvu zake kwenye harakati za ukombozi.
"Katika ziara hii pia tutavitembelea vyuo vikuu viwili alivyovianzisha kimkakati ambavyo ni Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na Chuo Kikuu cha Mzumbe.
"Kwenye elimu alifanya mambo mwengi lakini hatuwezi kutembelea yote tunachofanya ni kuhakikisha historia haipotei watoto wetu waliopo shule za msingi na wanaokuja waifahamu na watambue kilichofanywa na baba huyu wa taifa la Tanzania," alisisitiza Lupembe.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa idara ya mawasiliano, historia ya Mwalimu Nyerere kwenye elimu itaamsha chachu ya uzalendo kwa wanafunzi wa sasa na wajao katika kupata taifa la raia na viongozi bora.
No comments:
Post a Comment