Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Mwalimu Boniphace Maiga, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati waliyonayo ya kutunza na kulinda rasilimali misitu kwa kushririkiana na Program ya Kuendeleza Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC). (Picha na Suleiman Msuya).
Na Suleiman Msuya, Handeni
KATIBU Tawala wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Boniphace Maiga amesema wapo kwenye mkakati wa kutengeneza miundombinu
inayoingia kwenye misitu na vivutio vya utalii ili kuvutia watalii kufika kiurahisi.
Maiga amesema hayo wakati
akizungumza na waandishi wa habari waliokuwa wametembelea Msitu wa Asili wa
Tarawe uliopo katika Kijiji cha Tarawe Tarafa ya Mazingara wilayani hapo.
Waandishi
hao walitembelea msitu huo kupitia uratibu wa Program ya Kuendeleza Mnyororo wa
Mazao ya Misitu (FORVAC), inaofanya kazi katika wilaya 10 za Handeni, Kilindi,
Mpwapwa, Ruangwa, Nachingwea, Liwale, Namtumbo,Songea, Mbinga na Nyasa.
Akizungumzia
mipango hiyo Maiga alisema halmashauri itahakikisha inaboresha na kutengeneza
miundombinu mipya ambayo itasaidia watu wanaotembelea maeneo yenye vivutio
kufika kirahisi.
Maiga
alisema wilaya hiyo ina vivutio vya aina ya kipekee kama Pula Mbili (Pua
Mbili), Kungwi na Mwali, Nyoka wakubwa na misitu yenye mazingira mazuri.
Alisema
pia wilaya hiyo ndipo alipozaliwa Kibanga Kampiga Mkoloni hivyo waamini
uboreshaji na utangazaji wa vivutio hivyo utaongeza mapato ya vijiji na
halmashauri.
“Tunatambua
uwepo wa rasilimali nyingi vikiwemo vivutio vya utalii kama Pula Mbili, Kungwi
na Mwali, Nyoka Wakubwa na vinginevyo naamini tukiboresha mambo yataenda
vizuri,” alisema.
Katibu
Tawala huyo alitoa rai kwa wadau mbalimbali kujitokeza kushirikiana na FORVAC
katika kuhamasisha uhifadhi wa misitu ya vijiji pamoja na vivutio vilivyopo.
Diwani
wa Viti Maalum Halmashauri ya Handeni, Zawadi Bendera alisema atahakikisha
anafikisha changamoto za miundombinu kwenye hifadhi ya misitu na vivutio ili
kurahisisha kufikika kirahisi.
“Nitalifikisha
hili kwenye vikao vya halmashauri tutajadili lakini niombe Wizara ya Maliasili
na Utalii kuangalia fursa hii kwa jicho la huruma kwani miundombinu ikiboreshwa
tutapata fedha,” alisema.
Mratibu
wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msofe alisema iwapo halmashauri itaamua kutangaza
vivutio hivyo itaweza kuongeza mapato hivyo kutekeleza miradi ya maendeleo.
Msofe alisema watatumia Program ya FORVAC katika
wilaya 10 wanazotekeleza mradi kuhakikisha fursa zilizopo katika mnyororo wa
thamani ya mazao ya misitu inaongezeka.
No comments:
Post a Comment