HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 25, 2019

NMB yatoa misaada ya Mil. 70/- Geita, Morogoro

Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, wakimsikiliza Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Mashariki, Baraka Ladislaus, baada ya benki hiyo kukabidhi madawati 275 kwa shule tano za Kibwaya, Bwakila Chini, Newland, Kinole na Mfumbwe katika hafla iliyofanyika shule ya msingi Kibwaya. (Na Mpiga Picha Wetu).


Na Mwandishi Wetu



KATIKA utaratibu wake wa kila mwaka wa kutumia asilimia moja ya pato lake kwa miradi ya kijamii, Benki ya NMB imekabidhi misaada ya vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Sh. Mil. 70, kiasi kinachoifanya kufikisha zaidi ya Sh. Mil. 850 tangu mwaka huu uanze.


Misaada hiyo iliyotolewa wiki hii, ni kwa ajili ya Shule za Msingi, Sekondari na Zahanati wilayani Geita mkoani Geita na Halmashauri ya Morogoro mkoani Morogoro.


Hafla za makabidhiano ya vifaa hivyo, zilifanyika kwa nyakati tofauti, ambako Shule za Msingi Kilimani, Uhuru, Mchongomani, Shilabela na Nyakamwaga wilayani Geita, zilikabidhiwa madawati 274 yenye thamani ya Sh. Mil. 25, yaliyopokelwa na Mkuu wa Mkoa huo, Robert Gabriel.


Katika hafla hiyo, Gabriel pia alipokea kutoka kwa Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Abraham Augustino, mabati 348 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Kaseme na Kituo cha Afya Butundwe wilayani Geita, vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 10.


Huku akiishukuru NMB kwa msaada huo, Gabriel pia alipokea vitanda sita vya wagonjwa, kikiwemo kimoja kwa ajili kujifungulia akina mama wajawazito, pamoja na mashuka 50 na magodoro matano vyenye thamani ya Sh. Mil. 5 kwa ajili ya Zahanati ya Kashishi.


Augustino alisema kuwa, misaada iliyotolewa wiki hii, inaifanya NMB kutumia Sh. Mil. 850 kwa shughuli za kijamii kupitia Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ikiwa ni sehemu ya Sh. Bilioni 1 (ambayo ni sawa na asilimia 1 ya pato la mwaka), iliyotenga kwa miradi ya kijamii.


Katika Halmashauri ya Morogoro, Meneja wa NMB Kanda ya Mashariki, Baraka Ladislaus, ndiye aliyekabidhi msaada wa benki yake kwenda kwa shule za Kibwaya, Bwakila Chini, Newland, Kinole na Mfumbwe, zilizopewa madawati 275 yenye thamani Sh. Mil. 25.


Baraka aliwataka walimu na wanafunzi kwa kushirikiana na Kamati za Shule, kujenga utamaduni wa kutoa elimu ya namna ya kutunza madawati hayo.


“Tumetoa haya madawati 275 kwa shule tano na sisi kama NMB tutaona fahari kama madawati haya yanatunzwa na wanafunzi wa shule husika wakati Serikali na wadau wanatafuta mbinu ya kumaliza changamoto ya upungufu wa madawati na kuhamia kwenye changamoto nyingine,” alisema.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, alisema kuwa wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari kutosita kuwachukulia hatua wazazi wa wanafunzi ambao watabainika kuharibu miundombinu, ikiwemo kuharibu madawati makusudi.


“Agizo lililotolewa na Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo kwa wakuu wa shule la kuwataka wazazi kuchukuliwa hatua baada ya kubainika mtoto wake ameharibu miundombinu ya shule, ikiwemo kuharibu madawati kwa makusudi, lazima lifanye kazi sasa,” alisema Chonjo.

No comments:

Post a Comment

Pages