HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 24, 2019

OSHA YATOA SEMINA KWA WATU WENYE ULEMAVU WA KUTOSIKIA

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi OSHA, Khadija Mwenda, akizungumza katika semina iliyowashirikisha watu wenye ulemavu wa kutosikia.

Na Alodia Dominick, Bukoba

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco Gaguti ametoa wito kwa taasisi za serikali na zisizo za serikali mkoani humo kutoa ushirilikiano kwa Wakala wa Usalama na Afya Kazini (OSHA) ili wafikie malengo waliyokusudia.

Brigedia Gaguti ametoa wito huo wakati alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa semina ya siku moja iliyofanyika Manispaa ya Bukoba na kuwashirikisha watu wenye ulemavu wa kutosikia yaani viziwi.

Amesema, endapo watendaji wa serikali na mashirika binafsi watatoa ushirikiano kwa OSHA dhamira yao ya kuwafikia watu wenye ulemavu wa kutosikia utazaa matunda na hatimaye walemavu hao nao kuona ni miongoni mwa jamii ya watanzania.

"Serikali ya awamu ya tano imeweka dhamira ya kutekeleza sera ya viwanda inayolenga kuipeleka nchi katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, jitihada zimeendelea kufanyika katika utekelezaji wa sera hii ikiwamo ujenzi wa viwanda na uwekezaji katika miundo mbinu na miradi mikubwa ya kimkakati vyote kwa pamoja vinaajiri watu wengi wakiwemo walemavu"Alisema Brigedia Gaguti

Amewata walioshiriki semina hiyo kuweka agenda za maswala ya usalama na afya kwenye mikutano, matamasha na makongamano wanayoyafanya watenge muda mfupi wa kuongelea maswala haya kwani kundi la walemavu lipo katika hatari zaidi hasa kuweza kupata ajali au magonjwa yatokanayo na kazi.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda amesema wako Kagera kama sehemu ya mwendelezo wa programu ya kuwafundisha na kukutana na watu wenye ulemavu na sehemu ya kuwaweka tayari kwamba wao ni sehemu ya jamii.

Lengo la semina hiyo ni kuwafikia watu maalum na kuwa wao wanashughulika na usalama na afya mahala pa kazi.

Naye mwalimu  wa viziwi na mkalimani Barnaba Matuta amezitaja changamoto za viziwi kuwa ni mawasiliano baina yao na jamii inayowazunguka na hivyo akaomba ofisi zote za umma wapatikane wakalimani kwa watu wasiosikia.

No comments:

Post a Comment

Pages