Polepole amesema kuanza kwa safari hii ya kwanza
ya majaribio ni sehemu ya
Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020 katika eneo la usafiri na
usafirishaji wa watu na mizigo.
Miradi mikubwa mitatu inatekelezwa kwa
pamoja ikiwamo, ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa kutoka Dar mpaka Makutopola, Dodoma awamu ya kwanza, maboresho makubwa ya
reli ya kati kutoka Dar es Salaam mpaka Isaka ili kuiongezea ufanisi na ubebaji
mzigo mkubwa zaidi pamoja na ufufuaji na ukarabati mkubwa wa reli njia ya kaskazini
inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Kilimanjaro awamu ya
kwanza.
Treni hiyo ya abiria inayofanya
safari yake ya kwanza ya majaribio tangu iliposimamishwa kutoa huduma hiyo
miaka 25 iliyopita, imevutwa na kichwa cha kisasa cha treni '9013 Classic' na imefunga
mabehewa tisa yakiwamo mabehewa ya daraja la kwanza, daraja la pili, daraja la
tatu, behewa lenye mgahawa unaotoa vyakula vya aina yote, vinywaji baridi na vikali
pamoja na behewa la uendeshaji, usalama na usimamishaji wa treni.
Safari hii ya kwanza na ya kihistoria
imeleta hamasa, ambapo katika kila stesheni mamia ya wananchi walizuia
treni kwa shangwe, nderemo na vifijo.
Polepole amepongeza uongozi wa Shirika la Reli kwa kuipanga kwa
mafanikio safari hii ya kwanza ya treni ya abiria na ametoa rai kwa
vyombo vya ulinzi na usalama na Shirika kuimarisha ulinzi na kutoa elimu
ya ujirani wema kati ya reli na jamii ziishizo pembezoni mwa reli ili
kuitunza na kuilinda reli hii muhimu kwa maendeleo.
Pamoja na Polepole, watendaji wa Shirika la Reli wameongozwa na
Masanja Kadogosa ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TRC na Maafisa waandamizi kutoka Mamlaka
ya Usimamizi wa Usafiri wa Ardhini. (LATRA).
Imetolewa na,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
No comments:
Post a Comment