HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 18, 2019

NMB YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUKUZA UTALII

 Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Ndogo na za Kati wa Benki ya NMB-Filbert Mponzi akizungumza na wanachama wa chama cha waongoza watalii Tanzania (TATO) chenye lengo la kuihimiza ushirikiano kati yao.
Sehemu ya wageni waalikwa.
Mponzi akiwa na baadhi ya wageni waalikwa.
Mponzi akibadilishana mawazo   na baadhi  ya wageni waalikwa.


Na Mwandishi Wetu

BENKI ya NMB imeahidi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inasaidia harakati za Serikali kukuza Utalii nchini, ili kuinyanyua zaidi sekta hiyo ambayo inaongoza katika kuchangia pato la taifa na kuingiza fedha nyingi za kigeni ukilinganisha na sekta nyingine.
 
Ahadi hiyo ilitolewa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Ndogo na za Kati wa NMB-Filbert Mponzi, wakati wa Chakula cha Usiku, kilichoandaliwa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TATO) na kufadhiliwa na NMB, kikihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda.

Katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Arusha, Mponzi alibainisha kuwa, NMB imeshaanza kutoa mikopo ya magari kwa Waongoza Watalii ‘Tour Operators Vehicle Finance,’ lengo likiwa ni kuwawezesha waongozaji kurahisisha majukumu yao na kuvutia watalii zaidi na kukuza pato la taifa.

“Ni mikopo inayolenga kuwawezesha Waongoza Watalii kufanya biashara ya utalii bila kikwazo na kujiingizia kipato, ikiwa ni pamoja na kulinufaisha taifa kutokana na shughuli za utalii. NMB tumewekeza kwenye Sekta ya Utalii na imedhamiria kutoa rasirimali muhimu za kuwezesha ukuaji wa sekta hii.

Aliongeza kuwa, NMB wanashirikiana na Kampuni ya Hanspaul na RSA, huku akizitaja baadhi ya huduma walizojikita kuzitoa katika Sekta ya Utalii kuwa ni pamoja na ‘Asset Financing,’ Internet Banking, Makusanyo na Mapato ya TANAPA na NCAA na kurahisisha malipo kupitia Visa na Mastercard.

Kwa upande wake, Profesa Mkenda alikiri kuwa NMB ni wadau muhimu wenye mchango mkubwa katika ukuaji wa Sekta ya Utalii, ambayo inakua kwa kasi zaidi, hivyo akaipongeza benki hiyo kwa kushirikiana vyema na Serikali katika kukuza sekta hiyo.

Alifafanua kuwa, NMB imejipanga vya kutosha kuendeleza ushirikiano na Serikali pamoja na wadau katika kukuza Utalii nchini kwa kuwekeza zaidi kwenye sekta hiyo, ambayo ni kinara wa uchangiaji wa pato la taifa na kuingiza fedha nyingi za kigeni.

Mkenda aliwataja Benki ya NMB pamoja na TATO kuwa ni kati ya wabia muhimu katika maendeleo ya sekta hiyo na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana vyema na wabia hao ili kuibakisha Sekta ya Utalii kuwa vinara wa uchangiaji wa pato la taifa.

"Napenda kuwashukuru sana NMB kwa kuwezesha kufanikisha jambo hili, pia tumefurahi mnaiunga mkono Serikali, kwani nimesikia katika risala yenu kuwa mtaenda kule ambapo Serikali inaenda," alisema Profesa Mkenda.

Awali Mwenyekiti wa TATO-Willy Chambulo, alisema kuwa chama hicho kitaendelea kushirikiana na Benki ya NMB katika kukuza utalii na kuwawezesha waongoza watalii kutekeleza majukumu yao vema kwa ustawi wa sekta hiyo na ukuaji wa pato la taifa.
#NMBKaribuYako 

No comments:

Post a Comment

Pages