Na Mwandishi Wetu
SIKU chache baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa
serikali za mitaa uliosusiwa na vyama vya upinzani, Asasi za Kiraia zinazoangalia
uchaguzi Tanzania, (TACCEO) kimependekeza utaratibu wa mgombea kupita bila
kupingwa ufutwe.
TACCEO wamependekeza kuwa mgombea ambaye
hatakuwa na mpinzani apigiwe kura ya ‘Ndiyo au Hapana’ ili kuwapa wigo mpana
zaidi wananchi wa kumchagua kiongozi anayefaa.
Asasi hizo pia zimesema uchaguzi wa serikali
za mitaa uliofanyika Novemba 24, mwaka huu ulighubikwa na kasoro za kimfumo na
kiutendaji zilizowanyima wapiga kura, wagombea na vyama vya siasa haki ya
msingi ya kushiriki katika uchaguzi huo.
Akisoma tamko la TACCEO, mbele ya waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa asasi hizo Martina Kabisana, alisema wagombea uongozi
waliondolewa katika mchakato wa uchaguzi kwa madai yasiyokubalika kidemokrasia.
Kabisana, alisema licha ya kutimiza masharti
ya sheria na miongozo ikiwamo taratibu zinazotakiwa, asasi zinazounda
TACCEO na nyingine zilinyimwa vibali vya
kuangalia uchaguzi huo uliofanyika Novemba 24.
Alisema Sheria ya Serikali za Mitaa sura 287,
kama inavyoelekezwa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, inaeleza kuwa asasi
za kiraia zikitimiza masharti zingeruhusiwa kuangalia uchaguzi wa serikali za
mitaa uliofanyika Novemba 24 mwaka huu.
“Hatua hii kumeinyima haki ya kuangalia
uchaguzi pamoja na kumewanyima Watanzania haki ya kujua iwapo ulifanyika kama
kuaminika, huru na haki.
“baadhi ya wagombea bila kuwa na hadhi ya
uongozi wa umma, walipitishwa kuongoza vitongoji, vijiji na mitaa bila kupigiwa
kura; wanaongoza bila ridhaa ya wananchi, kinyume na msingi mkuu wa utawala bora
wa kidemokrasia, “ alisema Martina
“Tulikuwa na mipango na maandalizi ya teknolojia,
utaalam na mtaji wa kijamii kuangalia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu
kwa ufanisi nchini kote, na kisha kutoa ripoti,” alisema
Mjumbe wa TACCEO aliyeshiriki kusoma tamko
hilo Buberwa Kaiza, alisema kama serikali itaendelea kuwanyima vibali vya
kuangalia uchaguzi watangalia njia bora za kutekeleza wajibu wao.
Naye mmoja wa wajumbe wa TACCEO, Hebron Mwakagenda,
alisema wanapendekeza serikali na vyama vya siasa vishirikiane kuhakikisha
dosari zilizojitokeza hazijirudii tena kwa kuangalia mfumo wa usimamizi wa
uchaguzi.
“Tunaishauri serikali kwa kushirikiana na
wadau wengine, pamoja na vyama vya siasa, wakubali kuhamishia majukumu ya
kuandaa na kusimamia chaguzi za serikali za mitaa kwenye Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC)” alisema
TACCEO imependekeza kuwa elimu ya uraia kwa
wapiga kura, hususan katika serikali za mitaa, iwe ni suala la wakati ikiwamo
vyombo vya habari, asasi za kiraia kuendelea kutoa elimu hiyo.
No comments:
Post a Comment