Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (Mb), akizungumza jambo na Waziri wa Ushirikiano wa Biashara wa Finland, Mhe. Ville Skinnari, baada ya kumaliza mazungumzo alipomtembelea ofisini kwake, jijini Dodoma. (Picha na Wizara ya Fedha).
Na Peter Haule na Josephine Majula, WFM, Dodoma
Serikali imeuomba Umoja wa Ulaya (EU) kuwekeza katika
maeneo ya maendeleo ambayo tayari Serikali imeanza kuyatekeleza ikiwemo uboreshaji
wa miundombinu katika mkataba mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na EU kwa
mwaka 2021 hadi 2027.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti, kuhusu ushirikiano wa
maendeleo ya kiuchumi.
Dkt. Mpango alisema kuwa, katika mkataba mpya wa
ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na EU unaotarajiwa kuanza kutekelezwa
mwaka 2021 ni vema ukaendelea kuimarisha maeneo ya maendeleo ambayo tayari
yameanza kutekelezwa na Serikali hususani katika Sekta ya Elimu, Afya,
miundombinu na mingine ili kufikia malengo endelevu.
“Tuna kazi kubwa ya kuwekeza kwenye rasilimali watu
kwa kuwa miradi kama miundombinu haiwezi kufikia malengo yake bila kuwa na
uwekezaji katika rasilimali hiyo na ndio maana kama Serikali tumeamua kutoa
elimu bure kuanzia shule ya Msingi hadi Sekondari”, alieleza Dkt. Mpango.
Alisema kuwa katika suala la miundombinu, Serikali
inaangalia uwezekano wa kuanza ujenzi wa Reli kutoka Bandari ya Mtwara katika
Bahari ya Hindi hadi Bandari ya Mbamba Bay katika Ziwa Nyasa, ili kurahisisha
usafirishaji wa bidhaa na kuokoa fedha nyingi zinazotumika kukarabati barabara
zinazoharibika kwa usafirishaji wa bidhaa kwa njia ya barabara.
Aidha alieleza kuwa miundombinu hiyo ya reli itakuwa
na matawi kuelekea Liganga ambako kunapatikana madini ya Chuma na Mchuchuma
ambako kuna hazina kubwa ya Makaa ya Mawe.
Alisema Reli hiyo itasaidia pia kurahisisha
usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi jirani ikiwemo Malawi, hivyo kuchochoa
biashara na kuongeza mapato.
Kwa upande wake Balozi wa EU nchini Tanzania, Mhe.
Manfredo Fanti, aliipongeza Serikali kwa kuwa na Sera nzuri za maendeleo lakini
pia akasema kuwa ili kuboresha mazingira ya kibiashara, miongoni mwa mambo
yanayohitajika ni pamoja na Miundombinu, mafunzo, kuwa na uchumi wa kidigitali
na siasa bora, mambo ambayo Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuyatekeleza.
Mkataba wa ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi
uliokuwa ukitekelezwa kuanzia mwaka 2014 unamalizika mwaka huu ilihali kwa sasa
kunatarajiwa kuwepo kwa majadiliano ya mkataba mwingine wa ushirikiano
unatarajia kuanza kutekelezwa mwaka 2021 na kumalizika 2027.
Katika tukio jingine, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango namekutana na mkufanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikianao wa
Biashara wa Finland, Mhe. Ville
Skinnari, ambapo walijadili mambo mbalimbali yakiwemo masuala ya ushirikiano na
maendeleo ya kiuchumi.
No comments:
Post a Comment