HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 28, 2020

UFARANSA YATOA EURO MILIONI 1.49 KUSAIDIA KILIMOHAI

Na Irene Mark, Zanzibar
SHIRIKA la Maendeleo la Ufaransa limetoa Euro milioni 1.49 kufadhili shughuli za Kilimohai kwenye nchi tatu za Afrika ambazo ni Tanzania, Uganda na Comoro.
Fedha hizo asilimia 90 ya jumla ya Euro milioni 1.6  zilizotolewa na wafadhili mbalimbali ili kuhamamsisha kilimohai kwenye nchi husika.
Akizindua Mradi wa Ubunifu wa Kitaasisi kuhusu Kilimohai, Waziri  wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar,  Balozi Amina Salum Ali alisema wapo kwenye mchakato wa kutengeneza sera zitakazokitambua kilimohai.
Balozi Amina alisema mradi huo ni muhimu katika kuendeleza kilimo hai visiwani hapa huku akichajihisha kwamba watazingatia mnyororo wa thamani kuanzia maandalizi ya shamba hadi kumfikia mlaji kwa kuwa na mazao ya viwango bora ili kukamata soko kimataifa.
“Hivi sasaZanzibar tunatayarisha sera zitakazoshughulikia masuala yote ya kilimohai lakini pia tutakuwa na kituo cha viungo na mafuta ya majani asilia… lengo ni wakulima wetu wadogo ambao wengi ni wanawake kupata soko na kufanya kilimo kisichokuwa na gharama chenye kutunza mazingira.
“…Uzinduzi huu umekutanisha wataalam wa kilimo kutoka Serikali ya Muungano na hapa visiwani, pia tunao wabunge na kila mtu hapa amekiri kuunga mkono kilimohai na manufaa yake sasa ni Tanzania kufanya kilimo hiki ili kukamata soko la mazaohai yenye fursa ya mabilioni ya fedha nje ya nchi na wananchi wakila vyakula bora vyeye kulinda afya zao dhidi ya maradhi yasiyoambukizwa,” alisema Balozi Amina. 
Akizungumza wakati wa uzunduzi huo, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier alisema nchi yake itaendelea kusaidia Tanzania katika kilimohai kuhakikisha inakuwa mfano katika uzalishaji wa mazao pasipo kutumia kemikali.
Alisema mwaka 2021 wanatarajia kuingiza Zanzibar rasmi kwenye miradi ya kuendeleza kilimohai na kuongeza ufadhili ikiwemo kuwajengea uwezo wakulima kwa maendeleo endelevu.
“Kilimohai kinakabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kutunza mazingira, kinawezesha watanzania kukamata soko la dunia katika mazao mbalimbali,” alisisitiza Balozi Clavier.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa aliahidi kupeleka mjadala wa kilimohai bungeni ili kitengewe bajeti wakati wa mjadala wa bajeti ya kilimo kwenye kikao kijacho cha Bunge.
“Nawakaribisha TOAM mje bungeni kutuelimisha wabunge na mkija kwenye kamati yetu mtawafikia robo ya wabunge wote,” alisema Mgimwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mradi huo, Moses Aisu alisema kati ya fedha za mradi Tanzania itapata Dola 300,000 za Marekani na kwamba mradi huo utatekelezwa Zanzibar na Wilaya tatu za Tanzania Bara ambazo ni  Mafia, Dodoma na Ruvuma.

No comments:

Post a Comment

Pages