Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiongozana na Wakuu wa Vyombo vya
Ulinzi na Usalama kwenda kukagua maeneo
mbalimbali yanayosemekana yanatumika kupitisha wahamiaji haramu,ambapo serikali
imetangaza kuanza operesheni maalumu kudhibiti wahamiaji hao kipindi hiki nchi
ikielekea katika uchaguzi mkuu.
Afisa Uhamiaji Mkoa Kigoma,
Kamishna Msaidizi, Remigius Pesambili akisoma taarifa ya Utendaji kazi kwa
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (hayupo
pichani), wakati wa kikao cha ndani kilichohusiana na utendaji kazi wa Vyombo
vya Ulinzi na Usalama. Picha na Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi).
Na Mwandishi Wetu
Serikali imetangaza kuanza
operesheni, doria na misako maalumu ya
kuwasaka na kuwakamata wahamiaji haramu katika sehemu mbalimbali ikiwemo katika nyumba za kulala wageni, stesheni za mabasi, stesheni
za reli, mahoteli, mialo ya uvuvi pamoja na maeneo yenye muingiliano wa
shughuli za kibiashara hasa vijiji vinavyojishughulisha na shughuli za kilimo,makampuni
binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Hayo yamesemwa na Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, mkoani Kigoma baada
ya kikao cha ndani na Wakuu wa Vyombo vilivyopo chini ya wizara yake
ikiwemo Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Zimamoto na Uokoaji, Magereza, Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa(NIDA) na Idara ya Wakimbizi.
“Nchi yetu inaelekea
katika Uchaguzi Mkuu,kama vyombo vya ulinzi na usalama lazima tutimize majukumu
yetu na sasa tunaanza msako nchi nzima hasa katika mikoa iliyopo mipakani,tutaimarisha
vizuizi vyetu vya barabarani nchi nzima,tutatoa elimu kwa wananchi wetu jinsi
ya kuwatambua watu wasio raia ambao wameingia nchini bila kufuata utaratibu na
kubwa zaidi tutafanya ukaguzi katika makampuni binafsi na mashirika yasiyo ya
kiserikali” alisema Masauni
“kumekuwepo na wimbi
kubwa la watu kuingia nchini bila kufuata utaratibu,sisi kama serikali
hatukatazi mtu kuingia nchini basi wafuate utaratibu,kila mtu kwa kada yake
anaetaka kuingia nchini kuna utaratibu wake wa kufuata na serikali haijawahi
kumnyima raia yoyote yule wa kigeni fursa ya kuingia nchini.
Masauni pia aliwataka
wananchi kutowahifadhi au kuwasafirisha watu wasio raia kwani ni kinyume na sheria na
adhabu yake ni kifungo cha muda wa miaka ishirini au faini ya milioni ishirini au vyote kwa pamoja ikienda sambamba na
kutaifishwa kwa chombo cha usafiri kilichohusika kuwasafirisha washtakiwa na
kwa mwananchi atakaekutwa akimhifadhi au kumsafirisha mhamiaji haramu adhabu
yake ni kifungo kisichozidi miaka mitatu na faini isiyozidi laki tano au vyote
kwa pamoja.
Akizungumza katika
kikao hicho Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma,Kamishna Msaidizi Remigius Pesambili
alisema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba,2019 wamekamata wahamiaji
haramu 3.992 na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria”
“Idara ya Uhamiaji hapa
Kigoma kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama tumefanikiwa katika
mwaka uliopita kuanzia Januari hadi Disemba kukamata wahamiaji haramu kama
ifuatavyo; raia wa Burundi 3,293, Kongo 631, Kenya 12, Uganda 28, Rwanda 16, China
9, Somalia 2 na Msumbiji , ambapo jumla yake ni wahamiaji haramu 3,992 na
tayari washachukuliwa hatua na wengine wako magerezani tayari wakitumikia
adhabu” alisema DCI Pesambili
Aliongeza pia katika
kipindi cha Januari hadi Disemba 2019 raia wa kigeni 1,544 waliondoshwa
nchini,815 walipewa amri ya kuondoka,534 walifikishwa mahakamani,231 waliachiwa
huru baada ya kubainika kuwa hawana makosa ya kuwafikisha mahakamani na 868
walikabidhiwa Idara ya Wakimbizi.
Kuwepo kwa wahamiaji
haramu nchini kunatajwa kushamiri sana katika mikoa iliyopo mipakani huku
upatikanaji wa nyenzo za kutosha ikiwemo magari,elimu kwa wananchi juu ya kutoa
taarifa za wahamiaji katika eneo lao,utoaji wa vitambulisho vya taifa
uelekezewe nguvu hasa zaidi katika mikoa ya mipakani,vikao vya ujirani mwema
baina ya Tanzania na nchi tunazopakana nazo na utolewaji wa vibali vya
wakimbizi ikiwemo kufanyika upewaji wa uraia vikitajwa uenda vikawa suluhisho
la kupunguza uhamiaji haramu.
No comments:
Post a Comment