Katibu wa Chama cha mchezo wa Gofu Tanzania (TGU), Boniface Nyiti, akizungumza na waandishi wa habati jijini Dar es Salaam jana, kuhusu mashindano ya
Tanapa Gofu Lugalo Open 2020 yanayotarajiwa kufanyika Machi 14-15. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Klabu ya
Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali mstaafu, Michael Luwongo. (Picha na Francis Dande).
NA
CLEZENCIA TRYPHONE
ZAIDI ya wachezaji 100 wanatarajiwa kushiriki mashindano ya
Tanapa Gofu Lugalo Open 2020 yanayotarajiwa kurindima viwanja vya Gofu Lugalo jijini
Dar es Salaam, Machi 14-15 mwaka huu.
Mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka kwa udhamini wa
Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), ni kati ya yanayofana kutokana na idadi
ya washiriki na ushindani unaotolewa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Klabu ya
Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali mstaafu, Michael Luwongo, alisema mpaka sasa
zaidi ya washiriki 100 wamejitokeza tayari kwa kushiriki mashindano hayo ambayo
Waziri mwenye dhamana na michezo, Dk. Harrison Mwakyembe anatarajiwa kuwa mgeni
rasmi.
Alisema mashindano haya ambayo yako katika kalenda ya Chama
cha Gofu Tanzania (TGU), siku ya kufunga watazindua ofisi za mchezo huo ambazo
zipo Lugalo, ikiwa na lengo la kuweka sehemu moja mambo yahusuyo mchezo huo.
Aidha, Luwongo alisema kutakuwa na wachezaji wa hiari yaani
division A, B na C, watoto, wanawake na wanaume, ambapo kwa upande wa watoto
licha ya kuwa nao 70 mpaka sasa lakini 38 ndio watakaoshiriki katika mashindano
hayo.
Aliongeza kuwa, katika mashindano hayo wachezaji binafsi
wanaruhusiwa kujitokeza kushiriki huku akiwataka Watanzania kujitokeza kwa
wingi kuja kushuhudia mashindano hayo.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Tanapa, Hassan Mbaga,
alisema wao kutokana na jukumu lao la kutangaza utalii kupitia mchezo wa Gofu,
waliona ni njia sahihi za kuzidi kutangaza hifadhi mbalimbali zilizopo nchini.
"Tuna mwaka wa tatu sasa na tutaendelea kushirikiana na
Gofu katika kutangaza utalii kupitia hifadhi zetu, kwani mpaka sasa tuna jumla
ya hifadhi 22 wakati awali tulikuwa nazo 16," alisema.
Naye Nahodha wa Gofu Lugalo, Japheth Masai, alisema
maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika kwa viwanja kufyekwa tayari kwa
mashindano.
Alisema, Ijumaa wataanza wachezaji wa kusherehesha huku
wachezaji chini ya miaka 18 wakipepetuana Jumamosi asubuhi na walengwa wao
wakiumana Jumamosi na Jumapili.
No comments:
Post a Comment