HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 30, 2020

BMT kuandaa muongozo kuhusu ukomo wa wachezaji wa Nje nchini

Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo wa Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw.Yusuph Singo akifafanua kuhusu usajili wa wanamichezo wa kigeni hapa nchini leo Aprili 29, 2020 Jijini Dodoma.
 

Na Shamimu Nyaki, WHUSM-Dodoma
 
Serikali haijatoa ukomo wa wachezaji kutoka nje kushiriki michezo hapa nchini bali imeibua mjadala kwa wadau ili
watoe maoni yao.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara
ya Maendeleo ya Michezo Bw.Yusuph Singo kutoka Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwa ni hatua ya
kuboresha na kuimarisha sekta ya michezo nchini.
 
Ili kutekeleza mjadala huo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT)
limepewa jukumu la kuendelea kuandaaa mwongozo
utakaotumika kukusanya maoni kutoka kwa wadau kuhusu
ukomo wa wanamichezo wa nje hapa nchini.

“Katika Hotuba ya Bajeti iliyosomwa hivi karibuni Bungeni
jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe, hakuongolea idadi ya wachezaji kutoka nje wanaotakiwa kucheza nchini, bali
aliagiza BMT kuandaa mjadala mpana katika kukusanya maoni kwa wadau wa michezo kuhusu namna bora ya kusajili
wachezaji wa kigeni katika michezo yote hapa nchini” alisema
Bw. Singo.

Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo ambainisha kuwa
Mhe.Waziri Dkt. Mwakyembe alisisitiza kuwa wanamichezo
wote kutoka nje ya nchi wanaosajiliwa hapa nchini ni lazima
wawe na ubora pamoja na viwango vinavyotakiwa.

Akifafanua suala hilo Bw. Singo amesema kuwa michezo yote
ya kulipwa kwa sasa imeendelea kukua duniani kote na nchi
yetu pia inayo wachezaji wengi wanaocheza michezo hii
ikiwemo Mpira wa Kikapu (Basketball), Kriketi, Mpira wa
Miguu na michezo mingine, hivyo, Serikali haijatoa maelekezo ya ukomo wa usajili wa idadi ya wachezaji bali inataka kuwepo kwa mjadala wa wazi utakaotoa mwongozo wa ukomo wa idadi ya usajili wa wachezaji wa kigeni.

Aidha, Mkurugenzi huyo alitoa rai kwa wadau wa michezo nchini watakapopata fursa ya kuchangia au kutoa maoni katika mjadala huo wasiegemee katika timu wanazoshabikia, bali watoe maoni ambayo yatasaidia kuendeleza michezo na kuendeleza vipaji vya wanamichezo wetu pamoja na kukuza michezo nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages