Na Denis Mlowe, Iringa
MKUU wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi amelitaka jeshi la polisi
kwa kushirikiana na afisa biashara wa mkoa kufanya msako mkali kwa
wafanyabiashara wanaopandisha bei ya sukari na kuwa kinyume na bei elekezi
iliyotolewa na serikali.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada wa vitu mbalimbali vya
kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona vilivyotolewa na wadau mbalimbali
wa maendeleo juzi, Hapi alisema kuwa kuna wafanyabiashara ambao wamekuwa
wakipandisha bei na kwenda tofauti na bei elekezi.
Alisema kuwa serikali ilitangaza bei elekezi ya sukari hivyo
msako huo ufanyike kuweza kuwabaini wafanyabiashara hao kwa kuwa wanaenda
kinyume na kauli ya serikali ambayo imekuwa mstari wa mbele kuwatetea wananchi
wake kuondokana na kupandishwa kwa bei ya bidhaa.
Alisema kuwa mara kwa mara kikifika kipindi cha mfungo wa
ramadhani wafanyabiashara wamekuwa wakipandisha bei ya bidhaa mbalimbali hali
ambayo serikali haiwezi kukubaliana nalo kwani hali ya sukari iko salama kabisa
nchini tofauti na wafanyabiashara wanavyofanya.
Akizungumzia msaada aliotolewa na wadau wa maendeleo mkoani
hapa wakiongozwa na Kampuni ya Asas, Kampuni ya Qwihaya, Sai Energy na Taasisi
ya Cliton Foundation ambao wametoa misaada ya Barakoa, dawa na vifaa tiba,nguo
maalum za madaktari na waaguzi. Sabuni za maji, tanki za kunawia , themoscanner
na vitakasa mikono.
Alisema kuwa msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza
kupambana na maambukizi ya virus vya corona mkoani hapa na kuwashakuru kwa
kuweza kuvitoa kwa wakati mwafaka ambapo dunia inapambana kuweza kutokomeza
virusi hivyo.
Alisema kuwa katika kupambana na virusi hivyo wananchi
wanatakiwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu na kuwataka ofisi za serikali zote
mkoani hapa kuvaa barakao, kunawa mikono na vitakasa mkono na kutowahudumia
wananchi ambao hawajavaa barakao hadi wavae.
Alisema kuwa kila taasisi, na ofisi za watu binafsi
wazingatie maagizo ya serikali kwa kuweka vifaa vya usafi na sehemu za starehe
kuwe na utaratibu maalum kwa wateja wao na kuacha kuwa na mikusanyiko usiyo na
maana.
Aidha Hapi aliwataka watendaji kuwafatilia walimu na wazazi
ambao wameanzisha masomo kwa watoto majumbani na kufanya mikusanyiko
iliyokatazwa na serikali na Latra na vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia
uvaaji wa barakao na unawaji wa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka katika
vyombo vya usafiri, mabaa na hoteli.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni ya Qwihaya
inayojishughulisha na uuzaji wa magogo yenye makao makuu wilaya ya Mufindi, Leonard
Mahende alisema kuwa baada ya janga la Corona kampuni hiyo imewiwa na
kuweza kutoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh. Milioni 10.
Alivitaja vitu vilivyotolewa na kampuni hiyo kuwa ni simtank
60 zenye ujazo wa lita 250,vitakasa mikono, mavazi maalum kwa ajili ya
matabibu, sabuni za maji, thermometer na
lengo la msaada ni kuweza kusaidia wananchi na wauguzi waweze kutuhudumia kwa
usalama zaidi.
Aidha alitoa msaada wa vitakasa mikono kwa wanahabari wa
mkoa wa Iringa ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhabarisha umma juu ya
masuala mbalimbali lakini wakisaulika katika mambo mengi ya kijamii.
No comments:
Post a Comment