HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 24, 2020

ZEC YATOA TAARIFA KUHUSU UCHAGUZI MKUU 2020

Na Mauwa Mohammed, Zanzibar

TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inatarajia kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambapo wananchi watapata fursa yakumchagua Rais wa Zanzibar wajumbe wa baraza la Wawakilishi na Madiwani.

Akiwasilisha taarifa hiyo kwa vyombo vya habari Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Hamid Mahmoud alisema maandalizi ya uchaguzi huo yamegawika katika sehemu tatu.

 “Upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya uchaguzi, uandikishaji wa wapigakura wapya na uhakiki wa tarifa za wapigakura, kazi ya kufanya mapitio na idadi ya majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi “alisema Jaji Mahmoud.

Hata hivyo alisema kuwa Tume ipo katika hatua ya mwisho ya upatikanaji wa vifaa vya uchaguzi.

“Nachukua nafasi hii kuwafahamisha kuwa Tume imekamilisha uchapishaji wa nyaraka, uagiziaji na ununuzi wa vifaa mbali mbali vya uchaguzi na baadhi ya vifaa hivyo vimeshakabidhiwa Afisi ya Tume ya Uchaguzi.”alisema

 Mwenyekiti huyo wa Tume ambaye pia ni  Jaji Mkuu Mstafu alisema kazi ya uandikishaji wa wapiga kura wapya na uhakiki wa taarifa za wapigakura waliokuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ilianza tarehe 18/1/2020 katika Wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba.

Aidha kazi hiyo ilikamilika Mach  15 mwaka huu  katika Wilaya ya Mjini Unguja.

Katika kazi hii Tume iliandikisha wapiga kura wapya waliofikia umri wa kupiga kura. 

Aidha, ilifanya uhakiki wa wapiga kura waliokuwemo katika Daftari la wapiga kura tangu lilipoanzishwa mwaka 2005 na wapiga kura wengine ambao waliandikishwa kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2010, 2013 na 2015.

 Lengo la uhakiki wa wapiga kura ni kufahamu wapiga kura ambao wamepoteza sifa za kuwemo katika Daftari na kuwafuta waliokosa sifa.

Sambamba na hilo kazi ya uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura kwa ujumla ilikwenda vizuri  ingawa kulikuwepo na tatizo la baadhi ya Wananchi kukosa kuandikishwa au kuhakikiwa taarifa zao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

 Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar tayari imefanya tathmini ya kazi ya Uandikishaji ili kufahamu kwa kiasi gani zoezi hilo limetekelezwa.

 Hivi sasa Tume inaandaa utaratibu utakaowawezesha wananchi wenye sifa ambao walikosa fursa ya kuandikisha na kuhakiki taarifa zao ili wapate nafasi ya kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu ujao.

 Aidha, Afisi za Tume ya Uchaguzi za Wilaya hivi sasa zinapokea maombi ya wapiga kura wanaotaka kufanyiwa uhamisho wa taarifa zao kutoka vituo vya majimbo waliyopiga kura katika uchaguzi uliopita kwenda katika vituo vya majimbo ambayo wanaishi hivi sasa ambako watakuwa wametimiza sifa ya ukaazi katika vituo vya majimbo hayo.
 Kazi hiyo itaendelea na itasita miezi mitatu kabla ya upigaji wa kura. 

Tume imewaomba wale wote wanaotaka kufanya uhamisho wa taarifa zao kufanya hivyo muda huu vyenginevyo watalazimika kwenda kupiga kura katika vituo vyao vya zamani.

 Katika zoezi la awali la uandikishaji wa wapiga kura wapya na uhakiki wa wapiga kura, Takwimu za awali zinaonesha kwamba jumla ya wapiga kura 413,444 walipatiwa huduma hiyo vituoni na kati ya hao  wanaume walikuwa ni 199,327 na wanawake ni 214,117.(takwimu hizo ni za awali).

 Kazi nyengine ambayo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inawajibika kuifanya katika kipindi hiki cha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ni kupitia (review) idadi, majina na mipaka ya majimbo ya Uchaguzi. 

Kazi hii itafanywa na Tume kwa maelekezo ya kifungu cha 120(4) cha Katiba ya Zanzibar ambacho kimeipa uwezo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar katika kipindi cha miaka 8 hadi 10 au wakati mwengine wowote, kuchunguza idadi ya mipaka na majina ya majimbo hayo kwa kiwango kile ambacho Tume inahisi kuwa ni wajibu kuangaliwa upya na inaweza kubadili idadi, mipaka na majina ya majimbo hayo kadiri itakavyoona inafaa.

 Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar mara ya mwisho ilifanya mapitio kama haya ya majimbo mwaka 2015 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, mapitio ambayo yalipelekea kuongezwa kwa majimbo ya uchaguzi kutoka 50 yaliyokuwepo kabla na kuwa majimbo 54 yaliyotumiwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.

 Tume inawajibika kufanyia tena mapitio ya majimbo haya miaka mitano baada ya zoezi la mwaka 2015 kutokana na malalamiko katika baadhi ya majimbo ambako kuna wadi ambazo Shehia zake zinahudumiwa na majimbo mawili tofauti kinyume na utaratibu.

 Kwa kawaida kila jimbo linaundwa na wadi mbili mpaka tatu ambapo kila wadi inaundwa na shehia mbali mbali zilizomo katika eneo la uchaguzi.

Katika kazi ya mapitio ya majimbo ya mwaka 2015, kuna mkanganyiko ulijitokeza katika wadi na majimbo ya uchaguzi Unguja na Pemba.

 Kutokana na hali hiyo, Tume imeamua kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020 ifanye mapitio ya majimbo na ikiwezekana kwa mamlaka iliyo nayo ifanye marekebisho yanayostahiki kwa eneo ambalo linastahiki kufanyiwa marekebisho yanayofaa.

 Mapitio ya idadi na mipaka ya majimbo ya uchaguzi ni kazi shirikishi ingawaje mamlaka ya kufanya kazi hiyo kisheria ni ya Tume ya Uchaguzi.

 Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuthamini uwepo mkubwa wa wadau wa uchaguzi vikiwemo vyama vya siasa, Asasi za kiraia na mtu mmoja mmoja, inatoa nafasi kwa wadau wote kushiriki kikamilifu kutoa maoni na maono yao kwa njia ya barua au mawasiliano yoyote kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar juu ya hali ya majimbo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

 Maoni na maono hayo yatapokelewa katika Ofisi zote za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Unguja na Pemba wakati wowote baada ya kutoka kwa taarifa hii.

 Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilipanga kuchukua maoni ya wadau juu ya suala hili kwa kufanya mikutano mbali mbali na wadau.

 Hata hivyo, kutokana na maradhi ya homa ya mapafu (COVID 19) yanayosababishwa na virusi vya CORONA yaliopo nchini na kutokana na agizo lilitolewa na Serikali juu ya kujikinga na maradhi hayo kwa kuepuka mikusanyiko ya watu, Tume haitoandaa mikutano ya maoni, badala yake itapokea maoni na maono hayo kwa njia ya barua katika Afisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi iliyopo Maisara Unguja.

Na pia, Afisi ya Tume ya Uchaguzi Pemba iliyopo Chake Chake au katika Afisi za Wilaya za Tume zilizopo katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment

Pages