HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 02, 2024

TRC yaanza kutoa huduma kupitia treni ya mchongoko


 

Na Mwandishi Wetu

 

Shirika la Reli Tanzania (TRC) leo limeanza rasmi kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria kwa Mikoa ya Dar es salaam na Dodoma kupitia treni yake mpya ya mchongoko (Electric Multiple Unit-EMU)kupitia reli ya kisasa ya SGR ambayo inatajwa kwenda Kasi zaidi na kuokoa muda wa safari.

 

Akizungumza kabla ya kuanza kwa safari hiyo kutoka Stesheni ya Magufuli Jijini Dar Es Salaam kuelekea Dodoma leo Novemba 1, 2024 Mkurugenzi Mkuu wa TRC,Masanja Kungu Kadogosa amesema kuanza kwa safari kupitia treni hiyo ni hatua muhimu katika historia ya sekta ya usafirishaji hapa nchini.

“Leo tumeanza rasmi kutoa huduma kupitia treni hii na muhimu zaidi ni kwamba tumeongeza huduma zetu kwani mwitikio wa wananchi kutumia treni zetu za SGR umekuwa mkubwa sana  na wamekuwa na matumaini makubwa nasi hivyo kupitia treni hii ya mchongoko ni wazi huduma zetu zimetanuka zaidi”amesema.

 

Amesema kuwa treni hiyo ya moja kwa moja ( Express) itakuwa na ruti nne za kwenda Dodoma na nne za kurudi Dar es Salaam kwa siku ambapo treni hiyo ina madaraja mawili likiwemo daraja la biashara (business Class) na daraja la kifalme (Royal Class) ambapo nauli yake itakuwa ni shilingi za kitanzania 120,000 kwa abiria wa Dodoma-Dar na Dar-Dodoma.

 

Akitaja tofauti ya treni ya mchongoko Electric Multiple Unit-EMU na treni nyingine za SGR amesema kuwa treni hiyo inaokoa mpaka dakika 40 zaidi katika safari kwa kwenda kwa haraka zaidi huku muonekano wake ukiwa ni wa kuvutia ambapo haina kichwa bali kwenye behewa la abiria la treni hiyo pia Kuna sehemu ya dereva.

 

Aidha ameongeza kuwa treni hiyo ya mchongoko imezingatia walemavu wa aina zote na pia ina sehemu maalum kwa ajili ya akina mama kuwabadilishia watoto nepi (diapers) na eneo maalum kwa ajili ya kuwanyonyesha watoto.

 

Amesema treni nyingine za SGR pia zinaendelea kutoa huduma kama kawaida ikiwemo ya Dar es salaam -Morogoro.

 

 “tayari treni nyingine mbili za mchongoko zipo tayari na muda wowote uhitaji zaidi utakapoongezeka sisi tutazileta yaani watanzania wakitubipu sisi tutawapigia”amesema.

 

SGR ni ufupisho wa neno la kiingereza “Standard Gauge Railway”.Ni reli ya kisasa yenye upana wa mita 1.435, na inayopatikana duniani kote kwa zaidi ya asilimia hamsini na tano (55%).

 

Tofauti na reli ya kawaida, reli hii inaweza kusafirisha uzito mkubwa na kusafiri kwa mwendo kasi.

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia shirika la reli Tanzania (TRC) imeazimia kujenga reli hii ya kisasa kueneza mtandao usiopungua km 2,561 ikiunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Katavi na nchi zinazokuwa na bandari (Rwanda, Burundi, DRC).

 

SGR ni reli ya kisasa na ya kwanza Africa mashariki na kati itakayokuwa na uwezo wa kupitisha treni zitakazoendeshwa kwa nishati ya umeme na yenye mwendo kasi usiopungua kilometa 160 kwa saa.

No comments:

Post a Comment

Pages