·
Hatua kuchukuliwa kulingana na mahitaji ya Wateja
wa Biashara Ndogondogo na za Kati
·
Suluhisho pia kutolewa kwa Wateja Wakubwa
Dar es Salaam, Mei 21, 2020: Benki ya NMB Plc leo imetangaza unafuu wa ulipaji mikopo
kwa Wateja wa Biashara ndogo na za kati (SME/MSME) na wakubwa ili kuwasaidia kukabiliana
na madhara yaliyotokana na janga la COVID - 19 kwenye biashara zao. Hii ni jitihada
ya benki katika kutoa ahueni kwa wateja wake hususani sekta zilizoathiriwa zaidi
na janga la COVID-19.
Takribani wateja 412 biashara ndogo na za kati wameshapata ahueni hii kwa
kupitia likizo ya marejesho ya mikopo yao na wengine wakiongezewa muda wa
kulipa mikopo hiyo ili kuwasaidia kukabiliana na madhara yaliyoletwa na COVID –
19 katika biashara zao.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NMB , Ruth Zaipuna alisema athari ambazo
zimetokana na janga la COVID-19 kwa watu wa kawaida na wafanya biashara zimekuwa
si kubwa sana ukilinganisha na nchi ambazo zilifunga shughuli zote na watu kujifungia
ndani, hata hivyo, uamuzi wa nchi nyingine kujifungia umeleta mtikisiko katika
biashara duniani na hivyo kuathiri baadhi ya wateja wetu wa hapa nchini.
"Kama Benki, tunatambua kuwa huu ni wakati mgumu kwa wateja wetu ambao
biashara zao zimeathirika kutokana na mtikisiko huu kutoka nje, tumedhamiria
kutoa ahueni kutokana na mahitaji ya wateja na ukubwa wa athari, hii ni kwa sababu
si biashara zote na wateja wote wameathirika kwa kiwango sawa, mkazo ni katika
biashara zilizoathirika zaidi na COVID-19," aliongeza.
"Tunapenda kuwahakikishia wateja wetu kuwa hawako peke yao kwenye
safari hii. Milango yetu ipo wazi na tupo tayari kuwasaidia katika nyakati hizi
zisizo na uhakika za janga la COVID-19. Mara zote lengo letu ni kuhakikisha
ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Njia pekee tunayoweza kufanya hilo ni
kuhakikisha kuwa ukuaji wa wateja wetu ni endelevu, hivyo umuhimu wa kuwapunguzia mzigo huu katika
kipindi hiki”
“ Pamoja na ahueni hii ya kifedha, pia tutatoa mafunzo ya kibiashara na nasaha mbalimbali za uwekezaji na usimamizi
wa fedha kwa njia za kiilektroniki kwa kutumia wataalamu wa ndani." Alisema Bi. Zaipuna
Benki ya NMB pia imeimarisha njia mbadala za kidijitali ili kuhakikisha kuwa
mteja anafanya miamala kwa usalama mahali alipo, njia hizi ni kama NMB Mkononi na
miamala ya mtandao wa kompyuta inayotoa fursa ya kufanya miamala bila kufika
tawini.
Hatua hizo ni ushuhuda wa
kujitoa kwetu kupata suluhisho halisi, linalowalenga wateja, katika kipindi
hiki kisicho na uhakika, "alisema Zaipuna.
“Tunawasihi wateja wetu ambao wana uwezo wa kuendelea kufanya malipo yao, wafanye
hivyo. Hii itatuwezesha kupanua wigo kwa
wengine wengi ambao hawako katika nafasi sawa," alisema.
No comments:
Post a Comment