HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 22, 2020

KAMPUNI YA F.M ABRI YATOA NDOO KWA UMOJA WA DALADALA MANISPAA YA IRINGA

Mwakilishi wa kampuni ya F.M Abri, Yusuph Majariwa (kulia), akimkabidhi msaada wa ndoo maalum za kunawia mikono na sabuni za kutakasa mikono, Makamu Mwenyekiti wa umoja wa madereva daladala manispaa ya Iringa, Clement Duma kwa ajili ya mapambano dhidi ya maambukizi ya corona. (Picha na Denis Mlowe).


Na Denis Mlowe, Iringa

KAMPUNI ya F.M Abri ya mkoani Iringa inayojishughulisha na sekta ya usafiri wa mizigo na vituo vya mafuta imekabidhi ndoo maalum za kunawia mikono 30 na sabuni za kutakasia mikono zaidi ya 100 kwa chama cha madereva daladala manispaa ya Iringa ajili ya kupambana na ugonjwa wa corona.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya mkurugenzi wa FM Abri, Arifu Abri mwakilishi wa kampuni hiyo, Yusuph Majaliwa alisema lengo la kampuni hiyo ni kuiunga mkono serikali katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Alisema kuwa msaada huo umekuja baada ya maombi kutoka kwa mwenyekiti wa umoja wa madereva daladala manispaa ya Iringa, Ambakisye Mwangomba kuomba msaada huo hivyo wamekabidhi msaada wa ndoo maalum za kunawia mikono sabuni za kutakasa mikono.

Alisema kuwa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona ni muhimu kwa jamii kuungana na kuunga mkono serikali ya awamu ya tano katika janga hili ambalo limeikumba dunia na misaada kama hii inahitajika hasa kwenye huduma za usafiri.

Alisema kuwa kampuni hiyo imeendelea kusaidia jamii za mijini na vijijini kwenye mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona kwa kutoa misaada mbalimbali ya ndoo za kunawia mikono na sabuni za kutakasa na kutoa elimu kwa jamii.

Majaliwa alisema kuwa huo ni utaratibu wa kampuni ambao umewekwa kwa ajili ya kusaidia jamii na kurudisha faida  kwa jamii ambayo imekuwa ikiwaunga mkono katika shughuli za kila siku.

Lengo la kampuni ni kuunga mkono serikali katika mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona hivyo ni muhimu kutoa misaada kwa jamii yenye uhitaji hasa watu wanaohudumia watu kwa wakati mmoja ikiwemo sekta ya usafiri ambayo imekuwa ikihudumia jamii kubwa.alisema

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa waendesha daladala manispaa ya Iringa, Clement Duma akizungumza msaada huo aliipongeza kampuni ya FM Abri kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii na msaada huo umekuja katika wakati mwafaka na vifaa hivyo vitasaidia mapambano dhidi ya corona.

Alisema kuwa watahakikisha msaada huo wanatumia ipasavyo kwa kutoa elimu kwa abiria kuweza kunawa mikono na kutoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuzingatia maelekezo wanayopatiwa na wataalam wa afya kuweza kujinga dhidi ya maambukizi.

No comments:

Post a Comment

Pages