Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Ndg Milton Lupa akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi hiyo unaofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ujenzi mkoani Morogoro, leo tarehe 22 Mei 2020. (Picha Zote Na Mathias Canal, NFRA)
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wakifatilia mkutano unaofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ujenzi mkoani Morogoro, leo tarehe 22 Mei 2020.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Ndg Milton Lupa akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi hiyo unaofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ujenzi mkoani Morogoro, leo tarehe 22 Mei 2020. Wengine Pichani ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE NFRA Makao Makuu Mathias Mganga (Kushoto) na Katibu wa Baraza la wafanyakazi wa NFRA Ndg Jesse Mgana.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wakifatilia mkutano unaofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ujenzi mkoani Morogoro, leo tarehe 22 Mei 2020.
Na Mathias Canal, NFRA-Morogoro
Mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umejadili kwa kina ufanisi wa kazi pamoja na msisitizo kuhusu maslahi ya wafanyakazi.
Katika Mkutano wa Baraza hilo unaofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ujenzi mkoani Morogoro kwa siku mbili wafanyakazi wametoa maoni yao kuhusu umuhimu wa kushirikishwa katika shughuli mbalimbali mara kwa mara ili kutambua majukumu yanayofanywa na Taasisi hiyo.
Kadhalika wafanyakazi wa Wakala wameomba kuendelea kujengewa misingi ya uwajibikaji hasa katika kutambua wajibu wao kwa Umma na kusisitiza kuwa watattekeleza majukumu yao pasina uzembe katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizindua Baraza hilo jana tarehe 21 Mei 2020 Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Kilimo Bi Hilda Kinanga wakati akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya alisema si vema watumishi kutumia muda mwingi katika kufanya shughuli ambazo hazina tija zinazoathiri utendaji kazi.
Aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano inayo dhamira ya dhati ya kuondoa uzembe na ubadhirifu miongoni mwa watumishi wa umma na hivyo mtumishi anaruhusiwa kudai haki zile za msingi kwa kuzingatia Kanuni, Sheria na Taratibu za Utumishi wa umma wakati wa kutekeleza wajibu wake wa msingi kwa Mwajiri na kwa kutumia lugha ya staha.
Katika siku mbili za Kikao cha Baraza wajumbe wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu Wakala na miongoni mwa ajenda hizo ni Kupitia Mpango wa Biashara wa mwaka 2020/2021 (Business Plan), taarifa ya utekelezaji ya robo ya tatu ya mwaka 2019/2020 na kupitia Rasimu ya Miundo mipya ya Maendeleo ya Utumishi.
Wajumbe wamejadili kwa kina agenda hizo muhimu kwa kuwa agenda ya kwanza imewapitisha katika malengo/mipango ya Wakala, ya pili ni utekelezaji wa majukumu ya Wakala uliofanyika kwa mwaka tulionao na tatu ni mpango wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa lengo ya kuandaa majukumu mapya yanayoendana na Muundo mpya wa Taasisi.
Pamoja na kwamba wafanyakazi wa NFRA wamesisitiza umuhimu wa maslahi yao lakini kwa nyakati tofauti katika michango yao wamesisitiza kuwa hakuna haki bila wajibu hivyo wao wana wajibu muhimu wa kutekeleza majukumu yao na ari kubwa.
“Kwa kutambua uzito na umuhimu wa majukumu hayo kila mmoja wetu katika sehemu yake ya kazi anatakiwa kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa wananchi kwa kuwezesha nchi yetu kufikia uchumi wa kati” Amekaririwa Meneja NFRA Kanda ya Sumbawanga Ndg Abdillah Nyangasa
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Ndg Milton Lupa amesema kuwa bado Taasisi ina changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu ya kutoa huduma kwa umma ikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha na rasilimali watu wa kutosha, hali inayosababisha kutofikiwa kwa malengo.
Lakini amewahakikishia kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto hizo ikiwemo kuiomba itupatie watumishi ili kukidhi matakwa yetu.
Lupa amesisitiza kuwa Watumishi wote wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili katika Utumishi wa Umma. Aidha, Serikali haitasita kuchukua hatua kwa Mtumishi yoyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na vitendo vinavyokiuka maadili ya Utumishi wa Umma.
No comments:
Post a Comment