MSHAMBULIAJI wa Simba ya Dar es Salaam, John Bocco
amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Juni wa Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) msimu wa 2019/2020, huku Kessy Mziray wa Alliance FC akiibuka kuwa
Kocha Bora wa mwezi huo.
Bocco
alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Atupele Green wa
Biashara United na Martin Kiggi wa Alliance FC alioingia nao fainali
katika uchambuzi uliofanywa mwishoni mwa wiki na Kamati ya Tuzo za VPL
inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kwa
mwezi Juni, Bocco alikuwa na kiwango bora akiisaidia Simba kushinda
michezo miwili na kutoka sare miwili ikiendelea kubaki kileleni mwa
msimamo wa LigiKuu ya Vodacom, akipachika nyavuni mabao matatu katika
michezo minne aliyocheza. Simba iliifunga Mwadui mabao 3-0, ikaizamisha
Mbeya City mabao 2-0 ikatoka sare na Ruvu Shooting mabao 1-1 na ikatoka
0-0 na Prisons.
Atupele
Green aliingia hatua hiyo baada ya kuisaidia Biashara United katika
michezo mitatu ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu ‘hat trick’
katika mchezo dhidi ya KMC uliomalizika kwa Biashara United kushinda
mabao 4-0, wakati Kiggi aliingia hatua hiyo baada ya kutoa mchango
mkubwa kwa Alliance, ikishinda michezo miwili na kutoka sare mmoja, huku
Kiggi akifunga mabao mawili.
Pia
Kamati ya Tuzo, imemchagua Mziray kuwa Kocha Bora wa mwezi Juni
akiwashinda Sven Vandenbroeck wa Simba na Luc Eymael wa Yanga alioingia
nao fainali.
Mziray
aliiongoza timu yake katika michezo mitatu ikishinda miwili na kutoka
sare mmoja, ikipanda kutoka nafasi ya 18 hadi ya 14. Alliance iliifunga
Mbeya City bao 1-0, ikaifunga Coastal Union bao 1-0 na ilitoka sare na
Polisi Tanzania bao 1-1, wakati Vandenbroeck aliiongoza Simba kushinda
michezo miwili na kutoka sare miwili ikiendelea kubaki kileleni mwa
msimamo wa ligi, huku Eymael akiiongoza Yanga kushinda michezo miwili
na kutoka sare miwili ikiendelea kuwa nafasi ya tatu.
Wakati
huo huo, kikao hicho cha Kamati ya Tuzo kilichagua Kocha Bora wa Mwezi
Machi na Mchezaji Bora wa Mwezi Machi mwaka huu, ambao hawakuwa
wamepatikana licha ya ligi kuchezwa raundi nne hadi iliposimamishwa
katikati ya mwezi huo kutokana na tishio la ugonjwa wa homa kali ya
mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).
Kwa
mwezi huo Machi Mchezaji Bora alichaguliwa Meddie Kagere wa Simba
aliyeiongoza timu yake kushinda michezo mitatu na kupoteza moja ikibaki
kileleni mwa msimamo wa ligi, huku Kagere akifunga mabao matano, ambapo
Simba iliifunga Azam FC mabao 3-2, ikaifunga Singida United mabao 8-0
na ikaifunga KMC mabao 2-0 na ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 na Yanga.
Kagere
aliingia fainali na Paulo Nonga wa Lipuli aliyefunga mabao matatu na
Never Tigere wa Azam aliyetoa mchango mkubwa kwa timu yake ikiwa ni
pamoja na kufunga mabao matatu.
Kwa
upande wa kocha aliyechaguliwa ni Hererimana Haruna wa KMC aliyeingia
fainali na Vandenbroeck wa Simba na Khalid Adam wa Mwadui.
Hererimana
aliiongoza timu yake katika michezo mitano ikishinda minne na kupoteza
mmoja, ikipaa kutoka nafasi ya 19 hadi ya 15, ambapo KMC iliifunga JKT
Tanzania bao 1-0, ikaifunga Mbao FC mabao 2-0, ikaifunga Yanga bao 1-0
na iliifunga Alliance mabao 2-1, huku ikipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya
Simba.
Vandenbroeck
aliingoza Simba katika michezo minne ikishinda mitatu na kupoteza mmoja
na kubaki nafasi ya kwanza, huku Khalid Adam akiisaidia Mwadui kushinda
michezo mitatu na kupoteza mmoja ikipanda kutoka nafasi ya 16 hadi ya
12.
No comments:
Post a Comment