Na Mwandishi Wetu
CHAMA
cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimekubaliwa
kuwa mwanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Waandishi wa
Habari (IFJ).
Maombi ya
JOWUTA yalikubaliwa na IFJ katika kikao chake cha Kamati ya Utendaji
kilichofanyika Julai 9, 2020, jijini Brussels nchini Ubelgiji.
IFJ
inawakilisha waandishi wa Habari wapatao 600,000 katika nchi 140
duniani hivyo JUWUTA kupata uanachama ni hatua muhimu kwa waandishi wa
habari nchini.
Kwa mujibu
wa Mwenyekiti wa JOWUTA Claud Gwandu, chama hicho kiliwasilisha rasmi
maombi ya kujiunga na IFJ mwishoni mwa Juni, 2020.
"JOWUTA
inaamini katika mshikamano wa pamoja baina ya mwandishi wa habari
mmoja, vyama vya waandishi wa habari na kampuni za habari kwa kuwa ndiyo
njia sahihi ya kutatua changamoto zinazowakabili waandishi wa habari
nchini na duniani kote," alisema.
Gwandu
ameeleza kuwepo kwa faida kubwa kwa JOWUTA kujiunga IFJ kama taasisi na
kwa mwanachama mmoja mmoja hasa kipindi hiki ambacho sekta ya habari
duniani inakabiliwa na matatizo ambayo baadhi yake yanazuia waandishi wa
habari kutimiza majukumu yao.
"Baadhi
ya faida za JOWUTA kuwa mwanachama wa IFJ ni pamoja na wanachama wake
kupata fursa za kushiriki katika mafunzo, semina na mikutano mbalimbali
inayoandaliwa na shirikisho hilo moja kwa moja au kupitia ofisi yake ya
Afrika yenye makao yake makuu jijini Dakar nchini Senegal.
“Katika
kipindi hiki tunahitaji sana kuwajengea uwezo waandishi wanachama wetu
na waandishi wa habari kwa ujumla katika maeneo mbalimbali, kama
kuandika habari za uchaguzi kwa ufasaha, habari za maendeleo, sayansi na
teknolojia na kama inavyofahamika kuwa elimu ni ghali, hivyo nafasi hii
itasaidia kuongeza kasi ya kuwajengea wanachama wetu," alisema Gwandu.
Katika
barua yake, Katibu Mkuu wa IFJ Anthony Bellanger amesema shirikisho
hilo linafurahi kuona JOWUTA inajiunga katika umoja wa vyama vya
wafanyakazi vya waandishi wa habari na vyama vya habari duniani.
JOWUTA
ilisajiliwa rasmi Julai 26, 2018, ambapo Novemba 30, 2019 ilifanikiwa
kupata viongozi katika mkutano mkuu wa uchaguzi uliofanyika jijini
Dodoma.
Uchaguzi huo ulifanyika kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2006.
Kwa
sasa JOWUTA ina wanachama zaidi ya 300 waliopo katika mikoa mbalimbali
nchini, lakini pia tangu kusajiliwa kwake imefanikiwa kuendesha mafunzo
ya Usalama na Usawa wa Kijinsia kwa waandishi wa habari wanawake 204
katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mbeya, Iringa, Arusha,
Mwanza, Tabora na Tanga.
No comments:
Post a Comment