Mwanamichezo
Shija Richard Shija, amechukua fomu kuwania uwakilishi wa Jimbo la
Mbagala katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shija
ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga na Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha ya klabu hiyo, amechukua fomu
hizo katika ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Temeke, Dar es
Salaam.
Alifika katika
ofisi za CCM wilaya ya Temeke majira ya saa nane mchana. Hakutaka kutoa
maelezo zaidi ya kusema anasubiri taratibu za chama chake zichukue
mkondo wake.
"Siku kama
ya leo Julai 14, 1979 mama yangu alinizaa katika ardhi ya Mbagala.
Nikiwa Mwana wa Mbagala, najisikia furaha wakati ninapotimiza miaka 41
kujitoa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wenzangu wa Mbagala. Ni kweli
nimetoka kuchukua fomu. Chama chetu (CCM) kina utaratibu mzuri sana
kuhusu uchaguzi wa kura za maoni. Muda ukifika nitazungumza mengi. Kwa
sasa itoshe tu kuthibitisha kwamba ni kweli nimechukua fomu."
Shija
ni msomi wa Shahada ya Juu ya Uhasibu (CPA), pia ana shahada ya uzamili
(Masters) ya Sheria za Kodi na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
Alisoma elimu ya
msingi katika shule ya msingi Mbagala kuanzia 1988 hadi 1994. Mwaka 1995
alijiunga na sekondari ya Forodhani hadi 1998 alipohitimu na kujiunga
na sekondari ya Mkwawa iliyopo Iringa kwa masomo ya Juu ya Sekondari
mchepuo wa sayansi, PGM.
Pia
alipata kusoma Stashahada ya Juu Uhasibu kutoka chuo cha Uhasibu Arusha
(IAA) na Stashada ya Uzamili ya Usimamizi wa Fedha kutoka Chuo cha
Usimamizi wa Fedha IFM Dar es Salaam.
Mwaka
2017 aliwania Urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania na kushika
nafasi ya pili chini ya Rais wa sasa wa Shirikisho hilo, Wallace Karia.
No comments:
Post a Comment