*Asema lengo ni kuendelea
kujenga miradi ya kimkakati kwa maendeleo ya watu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe kabla ya kuweka
jiwe la msingi la upanuzi wa bandari ya Kasanga wilayani Kalambo, Julai
5, 2020. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipoweka jiwe la
msingi la upanuzi wa bandari ya Kasanga wilayani Kalambo, Julai 5, 2020.
Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim
Wangabo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino, Mhandisi Isack
Kamwelwe na kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Josephat
Kandege. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (kulia) ni Mbunge wa Sumbawanga
Mjini, Aeshi Hilaly baada ya kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa bandari
ya Kasanga wilayani Kalambo, Julai 5, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kudhibiti
matumizi ya fedha za umma ili iweze kuendelea na ujenzi wa miradi ya kimkakati
zikiwemo bandari kwa lengo la kuboresha maendeleo ya wananchi wake.
Pia, Waziri Mkuu amesema changamoto ya usafirishaji wa
mizigo na abiria kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
itakuwa historia baada ya kuboreshwa na kujengwa kwa miundombinu ya bandari
katika wa Ziwa Tanganyika ukiwemo upanuzi wa bandari ya Kasanga.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumapili, Julai 05,
2020) alipozungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa
upanuzi wa Bandari ya Kasanga iliyoko wilaya ya Kalambo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Rukwa. Mradi huo unagharimu
zaidi ya sh. bilioni 4.7.
Alisema upanuzi wa bandari hiyo utawezesha mizigo inayotoka
nchini kwenda Congo kufika kwa wakati kwa sababu itasafirishwa moja kwa moja
bila kupitia katika nchi nyingine kama ilivyo sasa, ambapo madereva
wanalazimika kupita kwenye Mataifa mengine na kutumia muda mrefu.
“Mradi huu ukikamilika utaongeza pato la mwananchi mmoja
mmoja pamoja na Taifa kwa ujumla. Rais Dkt. Magufuli amedhamiria kuboresha
maendeleo ya wananchi nchi nzima ikiwemo na wilaya hii ya Kalambo. Ujenzi wa
miradi hii unatoa fursa za ajira kwa wananchi, hivyo zichangamkieni.”
Vilevile, Waziri Mkuu alisema mapambano dhidi ya vitendo
vya rushwa bado yanaendelea nchini, hivyo mtu yeyote atakayebainika
anajihusisha na masuala hayo atafutwe popote alipo akamatwe na achukuliwe hatua
za kisheria kwa sababu rushwa ni adui wa haki.
Pia, Waziri Mkuu aliendelea kuwakumbusha watendaji ndani ya
Serikali wahakikishe wananchi wanapofika katika maeneo yao ya kazi wawapokee,
wawasikilize na kuwahudumia bila ya ubaguzi. “Hatuangalii sura wala kabila
yeyote atakayekanyaga kwenye maeneo yenu ahudumiwe ipasavyo.”
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack
Kamwelwe alisema Tanzania na Congo zimeungana kwa Ziwa Tanganyika, usafiri wa
barabara uliokuwa unatumika awali uliyalazimu maroli ya mizigo kupitia nchini
nyingine na kuchelewa kufika.
Alisema kukamilika kwa upanuzi wa bandari hiyo pamoja na
ujenzi wa barabara kwa kiwago cha lami kutoka Sumbawanga hadi Kasanga
kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kutumia bandari hiyo kuingia
nchini Congo moja kwa moja bila kupita kwenye nchi juirani.
Waziri Kamwelwe alisema kuwa awali kulikuwa na changamoto
ya barabara hali iliyosababisha meli kufika kwenye Bandari ya Kasanga na
kulazimika kusibiri mizigo ambayo ilikuwa ikichelewa kufika kutokana na ubovu
wa barabara na sasa tayari Serikali imeitatua kwa kuijenga kwa kiwango cha
lami.
Awali, akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Kaimu Katibu
Mkuu wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Uchukuzi,
Mhandisi Thomas Ngulima alisema mradi huo umeanzishwa ili kuongeza ushindani na
tija katika shughuli za kibandari kusini mwa Ziwa Tanganyika.
Alisema mradi huo unahusisha upanuzi mkubwa wa gati
ilililopo sasa lenye urefu wa mita 20 lifikie mita 120, ambazo zitawezesha
kuhudumia meli mbili hadi sita kwa wakati.
Kazi nyingine ni ujenzi wa miundombinu ya bandari ikiwemo jengo la kupumzikia
abiria, mgahawa na nyumba za watumishi.
Mhandisi Ngulima alisema mradi huo unaojengwa na kampuni ya
Inter-Consult Limited umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mwishoni
mwa mwezi Septemba, 2020 na kwamba utafungua na kuboresha njia ya biashara ya
mazao ya chakula katika nchi za DRC, Burudi na Zambia.
Aliongeza kuwa, ujenzi wa barabara ya kimkakati inayoanzia
Manispaa ya Sumbawanga hadi Kasanga (km 107), pamoja na upanuzi wa bandari
unaoendelea, utawezesha mtiririko wa shehena za saruji, makaa ya mawe, chokaa
na sabuni kuongezeka hivyo kukuza uchumi wa wananchi na Taifa.
No comments:
Post a Comment